1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je ni sahihi Chadema kujiondoa katika uchaguzi Tanzania?

Sylvia Mwehozi
8 Novemba 2019

Chama kikuu cha upinzani Tanzania CHADEMA kimejiondoa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, uliopangwa kufanyika mwishoni mwa Novemba. Hata hivyo hatua hiyo imezua mjadala kuhus mustakabali wa demokrasia.

Tansania Opposition Freeman Mbowe
Picha: DW/H. Bihoga

Chadema kilitangaza kwamba hakitoshiriki uchaguzi huo kikiorodhesha kasoro kadhaa zilizojitokeza. Hata hivyo, hatua hiyo imeibua mjadala mkubwa miongoni mwa wafuatiliaji wa siasa za Tanzania, kwamba nini mustakabali wa demokrasia katika taifa hilo?

"Chama chetu ni chama kikubwa na tuliweka wagombea wengi katika kila jimbo la uchaguzi. Tumeweka wagombea kwa asilimia 85 katika nafasi zote zilizokuwa zinagombewa ni asilimia 60 kutoka 85 ya wagombea wetu walioruhusiwa kupewa fomu, lakini hata hivyo bado walienguliwa hadi asilimia 8", alisema mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe kama alivyozungumza na DW kwa njia ya simu.

Malalamiko ya upinzani

Vyama vya upinzani kwa ujumla nchini Tanzaniavimeonekana kuwa njia panda kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, baada ya wagombea wake wengi kuenguliwa katika mazingira ya kutatanisha hatua ambayo imezusha hali ya sintofahamu katika uchaguzi huo. Vinadai kwamba hujuma hizo zinalenga kukipatia nafasi chama tawala CCM.

Ingawa CCM imekuwa ikiyakana madai hayo, wapinzani wamekuwa wakitoa orodha ya matukio ambayo yanaonyesha namna wagombea wao walishindwa kupitishwa kuwania nafasi ya uwenyekiti wa serikali za mitaa, kitongoji na vijiji.

Baadhi ya kasoro zinazolalamikiwa na upinzani ni kunyimwa fomu za serikali kwa wagombea wao, watendaji kufunga ofisi na kukataa kutoa fomu.

Wafuasi wa chama cha CCMPicha: DW/E. Boniface

Mwenyekiti wa chama cha CUF, Profesa Ibarahim Lipumba ameuita uchaguzi wa mwaka huu kuwa ni wa kituko akisema yale aliyoshuhudia hajapata kuyaona katika chaguzi zilizopita. Amemwomba Rais John Magufuli kuingilia kati ili kuwe na maridhiano kabla ya kufanyika uchaguzi huo.

Nacho chama cha NCCR Mageuzi kimesema kitakwenda mahakamani kupinga uchaguzi huo kutokana na kile wanachosema ‘kuvurugwa'.

Hata hivyo Waziri wa Tawala za mikoa na serikali ya Mitaa, Suleman Jaffo ambaye wizara yake inasimamaia uchaguzi huo amewatolewa mwito wasimamizi wa uchaguzi kutenda haki na ametaka rufaa za wagombea walioenguliwa kushughulikiwa haraka.

Upi ni mustakabali wa demokrasia?

Chama tawala CCM kinaonekana kufurahia hatua ya wagombea wake kupitwa bila kupinga na kujiondoa kwa Chadema katika uchaguzi huo, kunaweza kukipatia nafasi ya kushinda kwa wepesi. Je hatua waliyoichukua ni sahihi? Swali hili linajibiwa na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, kutoka Tanzania Prudence Karugendo.

"Maamuzi ya Chadema mimi naona yako sahihi kuliko chama kugombea, wakati chama tawala wamejiandaa kushinda uchaguzi huu kwa mabavu na kila aina ya mabavu."

Alipoulizwa kuhusu makosa wanayoyafanya wakati wa ujazaji fomu, Mbowe alisema kwamba " haiwezekani jiji la Dar es salaam lenye mitaa 570 wakaengua wagombea wote na kubakisha wagombea 24, Mbeya  asilimia 100 Arusha asilimia 100, haiwezekani! na hakuna mgombea wa CCM anayekosea kujaza fomu ila wa upinzani tu. Nakuhakikikishia hakuna mahali tumekosea ila ni makada wa CCM wanaowaondoa wagombea wetu."

Wafuasi wa chama cha Chadema Picha: DW/E. Boniface

Lakini swali kubwa ni kwamba ikiwa Chadema wanaamini hawakuwa na makosa katika utaratibu wa kujaza fomu, kwanini basi kisifuate mchakato wa kisheria wa kukata rufaa badala ya kugomea uchaguzi?

"Kanuni na sheria za uchaguzi katika hatua ya sasa hazitoi mwanya wa kwenda mahakamani kupinga matokeo au kusimamisha uchaguzi. Wasimamizi wa uchaguzi ndio hao hao wanahusika kuengua watu wetu."

Chadema imewatolea mwito watanzania na wafuasi wake wote kutota ushirikiano kwa serikali yoyote ya mtaa au kijiji iliyopatikana bila uchaguzi . Inasema hao waliopitishwa bila kupinga hawajafanyiwa kura wala kipimo chochote cha kukubalika kwao kwa wananchi. Tumesema hatuwezi kushiriki uchaguzi wowote ambao hausimamiwi na tume huru.

Uchaguzi wa serikali za mitaa unachukuliwa na vyama vya siasa kama kioo kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwakani. Tanzania itafana uchaguzi huu mwishoni mwa Novemba na uchaguzi mkuu mwaka 2020.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW