Je, ni sawa wanaume kutumia majina ya ukoo ya wake zao?
26 Septemba 2025
Uamuzi huu wa mahakama kuu wa kuruhusu wanaume kutumia jina la wake zao umezusha mjadala wa kijamii na kisaikolojia unaohusisha mila, desturi, haki za binadamu, na usawa wa jinsia, nafasi za kiasili za mume na mke ndani ya ndoa pamoja na mitazamo tofauti ya wananchi na dini kuhusu athari zake kwa familia za Kiafrika.
Mahakama imetangaza kwamba baadhi ya vifungu vya Sheria ya Usajili wa Kuzaliwa na Vifo havina msingi wa kikatiba kwa sababu vinawabagua wanawake na ujio wa sheria hiyo umetokana na shauri lililowasilishwa na wanandoa wawili walionyimwa ruhusa walipojaribu kuwasajili watoto wao kwa kutumia jina la upande wa mwanamke.
Jina la ukoo la mwanaume limekuwa alama ya utambulisho
Siyabonga Wanga Mtambo, mkaazi wa Mamelodi, anasema uamuzi huo wa Mahakama Kuu ni sawa na kudhoofisha utamaduni wao. ''Kwa kuleta sheria hii kwangu, ni kama wanadhoofisha utamaduni wetu kama watu weusi, hasa Waafrika. Unaweza kutembea barani Afrika kote, na sidhani kama mtu yeyote Afrika angeweza kuruhusu jambo hili,'' alisema Siyabonga.
Matamshi hayo yanaficha hisia za kutokuelewana ambazo uamuzi huu umeibua. Baadhi wanaona hatua hii kama njia ya kudumisha usawa wa jinsia, huku wengine wakiiona kama inayoharibu utamaduni wa Kiafrika.
Kwa maelfu ya miaka, desturi za familia zimetawala maisha ya Waafrika. Jina la ukoo la mwanaume limekuwa ni alama ya utambulisho, heshima, na urithi wa familia. Mahakama hiyo sasa inafungua mlango mpya, ikisema, kila mtu ana haki ya kuchagua jina lake, hata kutumia jina la ukoo la mke wake.
''Ni wakati wa mabadiliko, lakini pia ni changamoto. Tunapaswa kuzingatia mila zetu na utu wa familia. Kwangu mimi naona wamewakosea sana mababu zetu, huwezi chukua mkia uwe kichwa na kichwa kiwe mkia,'' alisisitiza Tinta Stevens, mkaazi wa Afrika Kusini.
Wataalamu wa sheria wanasema uamuzi huu ni mwanzo wa mageuzi ya kijamii, ambapo haki za binadamu na heshima ya kijamii vinaingiliana. Lakini kwa baadhi ya wananchi, hoja za utamaduni ni za kina zaidi. Thembisa Mbiyozo kutoka Afrika Kusini, anahisi kwamba hatua hii sawa na kupuuzia historia na mila ya Kiafrika.
Kulingana na Mbiyozo, kwake yeye inaonekana sasa wanaume hawatakuwa na thamani yoyote, na kama wanataka wanawake wawe vichwa vya familia, waweke sheria nyingine inayowaruhusu wanawake kutoa pia mahari. Mwananchi huyo anasema sheria hiyo itakapoanza kutumika, itakuwa mbaya zaidi.
Uamuzi huu unalenga kutoa uhuru wa chaguo binafsi
Mahakama Kuu ya Afrika Kusini imeeleza kuwa uamuzi huu hauuharibu tu utamaduni, bali unalenga kutoa uhuru wa chaguo binafsi, ikizingatia haki za binadamu. Lakini barani Afrika, mahusiano kati ya sheria na mila ni changamoto ya kila siku.
Padri Musa Malome, mmisionari wa Kanisa Katoliki nchini Afrika Kusini, anasema kwa upande wa Wakristo, suala hili halina pingamizi. ''Kuna baadhi ya makabila ambapo jina linalotawala ni jina la kike, mfano kule Tanzania kabila la Waluguru majina yote huwa upande wa mama, ndiyo maana wajomba wanakuwa na nguvu sana kwa sababu ndiyo wenye jina la ukoo. Kama Afrika Kusini wameamua iwe hivyo ni sawa tu, Mungu hakatai na halina pingamizi la kibibilia,'' alifafanua Padri Malome.
Kwa sasa, hoja na mjadala vinaendelea huku bunge la Afrika Kusini likiwa limepewa miaka miwili tu, kuhakikisha linafanya marekebisho katika Sheria ya Usajili wa Kuzaliwa na Vifo. Lakini maswali makubwa bado yako wazi, je, uamuzi huu utaathiri maisha ya familia za Kiafrika na jinsi zinavyojenga utambulisho wa vizazi, au utaacha kuwa mjadala tu wa hoja za kijamii na kisiasa? Muda wa sheria hii kuanza kutumika ukifika, bila shaka majibu ya maswali mengi yaliyojaa utata, yatapatikana.