1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, Orban atafanikisha lengo la kutatua mzozo wa Ukraine?

Angela Mdungu
9 Julai 2024

Siku kadhaa baada ya Hungary kupata nafasi ya uenyekiti wa baraza la Umoja wa Ulaya wa kupokezana kwa muda wa miezi sita, Waziri mkuu wa nchi hiyo Viktor Orbán ameshasafiri kwenda Kyiv, Moscow na Beijing.

Siasa | Umoja wa Ulaya | Hungary | Waziri Mkuu Viktor Orban
Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban akikagua gwaride la heshimaPicha: Stanislav Filippov/AP/picture alliance

Wakati akielekea Washington baada ya ziara alizozifanya Kyiv, Moscow na Beijing, huenda Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban akawa anatafuta ushirika na mgombea wa chama cha Republican Donald Trump, kama atachaguliwa kuwa Rais wa Marekani kwenye uchaguzi wa mwezi Novemba.

Kuna minong'ono kuwa huenda Waziri Mkuu huyo wa Hungary akakutana na Trump atakapofika Washington. 

Katika video aliyoichapisha katika jukwaa la X mapema Jumatatu, Orban katika ziara yake China, aliipongeza Marekani kuwa taifa pekee kubwa duniani lenyedhamira ya kurejesha amani kati ya Urusi na Ukraine. 

Katika video hiyo hiyo, alisikika akisema kuwa ziara hiyo ni muhimu kwa Hungary na Umoja wa Ulaya kwa ujumla. Aliongeza kuwa wataendelea kufanya kazi kwa pamoja. Ingawa hakuweka wazi kama anauwakilisha Umoja wa Ulaya, baadhi ya watu wanaamini kuwa alitaka ieleweke hivyo. 

Kaja Kallas, atakayeshikilia wadhifa wa mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya hivi karibuni alisema, Orban anatumia vibaya uenyekiti wa nchi yake katika baraza la Umoja huo na anajaribu kuleta mkanganyiko katika sera ya  Umoja wa Ulaya kuhusu Ukraine.

Soma pia:Waziri Mkuu wa Hungary , Rais Xi Jinping wakutana Beijing

Hata hivyo kwenye chapisho lake la Julai 5 katika jukwaa la X Viktor Orban albainisha kuwa hana mamlaka ya kufanya mazungumzo kwa niaba ya Umoja wa Ulaya.

Licha ya hilo, alisababisha mtafaruku alipoongeza kusema  "Hatuwezi kukaa na kusubiri vita viishe kimiujiza. Tutafanya kazi kama chombo muhimu cha hatua za mwanzo katika kuleta amani"

Umoja wa Ulaya ulimkaripia vikali baada ya kiongozi huyo kukutana na Rais Vladmir Putin na  kusema kuwa hauwakilishi Umoja wa Ulaya kwa namna yoyote ile.

Makamu wa Kansela wa Ujerumani Robert Habeck, alisema kuwa mikutano ya Orban inapaswa kuchukuliwa kama suala la nchi mbili na si siyo shughuli rasmi za Umoja wa Ulaya. 

Kwa mara nyingine tena hata hivyo Orban ameonesha kuwa ni mshirika tata katika Jumuiya hiyo yenye wanachama 27. Wataalamu wanasema anachokifanya sasa kiongozi huyo ni sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kujionesha kuwa kiongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia barani Ulaya, na kuwa anampigia upatu mgombea wa chama cha Republican wa Marekani Donald Trump kurejea madarakani. 

Orban ana madhumuni gani ya kisiasa EU? 

Hatua ya Waziri Mkuu wa Hungary kuonesha kuiunga mkono Urusi au uhusiano wake na Urusi si kitu kipya. Kwa zaidi ya miaka miwili , bila kutetereka amekuwa akipinga vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Moscow na amejaribu kuzuia misaada kwa Ukraine. Hata wakati huu umoja huo ukijaribu kujiweka mbali kibiashara na China, Budapest imeimarisha biashara na Beijing.  

Fahamu kuhusu uchaguzi wa Bunge la Ulaya

01:24

This browser does not support the video element.

Mshauri wa siasa na mtaalamu wa masuala ya Ulaya Julien Hoez anasema kuwa maigizo ya Orban ya hivi karibuni yanakusudia kumpa uungwaji mkono nchini mwake baada ya chama chake cha Fidesz kufanya vibaya katika uchaguzi wa Umoja wa Ulaya nchini humo mwezi uliopita.

Soma pia:Waziri Mkuu wa Hungary afanya mazungumzo na Rais wa Urusi Vladmir Putin

Kwa upande wake Profesa mwandamizi wa siasa za Ulaya na za kimataifa Pierre Haroche katika taasisi ya Jacques Delors amesema kuwa kwa sasa Orban anajiandaa kuwa mwezeshaji wa Trump barani Ulaya.

Anafafanua kuwa, waziri mkuu huyo wa Hungary anafanya maandalizi ya awali kwa ajili ya kupata makubaliano na Trump aliyewahi kusema kuwa anaweza kuumaliza mzozo wa Ukraine ndani ya saa 24.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW