Je Masood anaweza kumngoa Mwinyi madarakani?
29 Oktoba 2025
Uchaguzi mkuu huu unatarajiwa kushuhudia mapambano makali ya kihistoria kati ya daktari wa binaadamu na mtoto wa rais mstaafu, Hussein Ali Mwinyi wa CCM na mwanasheria mzoefu, Othman Masoud, maarufu kama OMO. Wote wawili wanabeba uzoefu wa utawala, ingawa wanatofautiana kimaono na kimitindo.
Kwa upande wake, Mwinyi anayetafuta muhula wa pili na wa mwisho ni daktari aliyebobea katika tiba ya magonjwa ya ndani, akiwa amepata shahada yake ya tiba kutoka Chuo Kikuu cha Marmara nchini Uturuki na shahada ya pili kutoka chuo kikuu cha King's College nchini Uingereza. Kabla ya siasa, alifanya kazi hospitalini na pia kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kairuki jijini Dar es Salaam:
Hussein Mwinyi alianza utumishi wa kisiasa upande wa Tanzania Bara, akiwa mbunge wa jimbo la Mkuranga mkoa wa Pwani na kisha kuingia serikalini alikohudumu kama naibu waziri na waziri kamili katika wizara mbalimbali tangu mwaka 2000. Baadaye aliwania na kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Kwahani kisiwani Unguja. Lakini wadhifa wake muhimu zaidi ulikuwa ni ule wa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa alioushikilia hadi anatangazwa kuwa rais wa Zanzibar kufuatia uchaguzi wenye utata wa mwaka 2020.
Alipoingia madarakani, alijipambanuwa kama kiongozi anayependa uwazi na ushirikishi akionesha kupambana dhidi ya uzembe na ufisadi serikalini, akiimarisha ujenzi wa miundombinu na akitangaza kuuinuwa uchumi kupitia sera ya uchumi wa bahari, ama Uchumi wa Buluu, kama ilivyojuilikana.
Mwinyi aliunda serikali yenye sura ya umoja wa kitaifa
Aliunda serikali yenye sura ya umoja wa kitaifa kwa kushirikiana na chama cha ACT Wazalendo, chama ambacho kinalalamikia kuwa matokeo ya uchaguzi uliomuweka Mwinyi madarakani hayakuwa sahihi. Hata hivyo, miezi michache baada ya kuanza kazi, wapinzani wake ndani na nje ya serikali walianza kumtuhumu Mwinyi kwa kuendeleza kile kile alichokuwa akidai kukipinga.
Kwa upande wa Othman Masoud Othman, Makamu wa Kwanza wa Rais wa sasa na Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, anawakilisha kambi ya upinzani akitumia rekodi yake ya utaalamu wa kisheria kama nguvu ya mageuzi:
Msomi huyu mwenye shahada mbili za uzamili katika sheria, alitumikia utumishi wa umma kwa miaka 25, akijipatia sifa kama mmoja wa Wazanzibari wachache wenye 'kumbukumbu ya kitaasisi' hasa katika masuala ya kisheria. Alikuwa muasisi wa Kurugenzi ya Mashtaka Zanzibar alipoteuliwa kuianzisha na kuwa mkurugenzi wake wa kwanza kutoka mwaka 2002 hadi 2011, ambapo alibadilisha mfumo wa uendeshaji mashtaka visiwani humo. Kisha alihudumu kama Mwanasheria Mkuu waZanzibarkutoka mwaka 2011 hadi 2014.
Kabla ya hapo alishakuwa naibu katibu mkuu, naibu mwanasheria mkuu, katibu mkuu, mwenyekiti wa bodi ya mapato na nafasi nyengine kadhaa ndani ya serikali na mashirika ya umma. Nafasi ya mwisho kabisa kabla hajaingia rasmi kwenye siasa ilikuwa ni ujumbe wa bodi ya Shirika la Hakimiliki la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi, akiwa mjumbe anayeiwakilisha Afrika.
Jina lake lilianza kujulikana zaidi kisiasa alipoondolewa katika nafasi ya Mwanasheria Mkuu mwaka 2014 kwa sababu ya msimamo wake mkali wa kutetea maslahi ya Zanzibar katika Bunge Maalum la Katiba. Baada ya kifo cha Maalim Seif Sharif Hamad, alipendekezwa na chama cha ACT Wazalendo kurithi nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar mnamo Februari 2021. Kisha akawa makamu mwenyekiti wa chama hicho upande wa Zanzibar kabla ya kupanda cheo na kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa ACT Wazalendo mwaka 2024.
Kwenye kampeni zake za urais zilizohitimishwa juzi Jumapili, Oktoba 26, Othman alikuwa anasisitiza umuhimu wa uwajibikaji, uadilifu, na utawala wa sheria.Anahimiza kuchagua viongozi jasiri watakaorudisha hadhi na haki za Zanzibar na kuondoa ufisadi. Mafanikio yake katika kuimarisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na kuanzisha Bodi ya Mapato Zanzibar, yanatumika kama vielelezo vya uwezo wake wa kuijenga na kuimarisha Serikali kitaasisi:
Kwa vyovyote vile, uchaguzi huu wa 2025 utakuwa mtihani wa aina yake: utaamua kama Wazanzibari wataendelea na sera za Mwinyi za kuendeleza ujenzi wa miundombinu na kukuza uchumi wa buluu au watamchaguwa Othman Masoud na ACT Wazalendo kwa ahadi za mageuzi ya kitaasisi na kusimamia sheria kama msingi wa maendeleo. Wote wawili ni viongozi wenye uzoefu wa juu, ingawa wanatoka katika nyanja tofauti kabisa za utendaji.