1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMamlaka ya Palestina

Je Palestina huchukuliwa kuwa taifa?

6 Novemba 2023

Kwa miongo mingi, swali la utawala wa Palestina limezusha mzozano kati ya wasomi, wanadiplomasia na mataifa binafsi.

Japo Palestina haizingatiwi rasmi kuwa dola, kwa miongo kadhaa, mamlaka yake imepeperusha bendera hii ambayo ni yao rasmi.
Japo Palestina haizingatiwi rasmi kuwa dola, kwa miongo kadhaa, mamlaka yake imepeperusha bendera hii ambayo ni yao rasmi.Picha: picture-alliance/dpa

Je, taifa au dola ni nini? Zipo nadharia mbili kuhusu utaifa: Nadharia ya kutangaza na nadharia ya kuunda.

Nadharia ya kutangaza dola

Wanaoamini nadharia ya kutangazwa wanasema eneo huweza kutazamwa kuwa dola ikiwa linaafiki maelezo ya utaifa kama ambavyo yameainishwa kwenye mkataba wa Montevideo wa mwaka 1933.

Mkataba huo unasema ili dola lizingatiwe, eneo lazima liwe na wakaazi wa kudumu, liwe na mipaka inayobainika, iwe na serikali na pia uwezo wa kuingia katika uhusiano ai mikataba na mataifa mengine.

Mkataba huo unafafanua kwamba kuwepo kwa serikali katika misingi ya kisiasa, hakutoshi kutambuliwa na mataifa mengine.

Soma: Jeshi la Israel lashambulia maeneo 450 katika Gaza

Mkataba huo unaeleza kuwa: "Hata kabla ya kutambuliwa, serikali ina haki ya kutetea uadilifu na uhuru wake, kutoa uhifadhi na ustawi wake, na kwa hivyo kujipanga kama inavyoona inafaa, kutunga sheria juu ya masilahi yake, kusimamia huduma zake, na kufafanua mamlaka yake na uwezo wa mahakama zake.”

Marekani ambayo ni mshirika wa karibu wa Israel na pia mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imetumia kura yake ya turufu kuzuia majaribio kadhaa ya mamlaka ya Palestina kuwa taifa.Picha: Timothy A. Clary/AFP/Getty Images

Nadharia kuhusu uundaji wa taifa

Tofauti na mkataba wa Montevideo, nadharia hii inasema eneo linaweza kuzingatiwa tu kama taifa ikiwa nchi nyingine za ulimwengu zitalitambua kuwa taifa. Nadharia hii haijaratibiwa kisheria: badala yake, inachukulia utaifa wa kisasa kama suala la sheria za kimataifa na diplomasia.

Wasomi wana mitazamo kinzani ikiwa mamlaka za Palestina zinaafiki kuwa taifa kwa mujibu wa ufafanuzi wa kisheria. Baadhi wanasema inaafiki, lakini wengine wanasema haikidhi matakwa ambayo yameainishwa kwenye mkataba wa Montevideo.

Soma: Palestina yaahirisha uchaguzi wa Bunge

Wengine wanapinga matumizi ya mkataba wa Montevideo katika kuamua suala la utaifa, wakihoji kuwa tumaini bora la Wapalestina kudai utaifa ni wao kutambuliwa kimataifa.

Kwa kuwa mamlaka ya Palestina si nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa, haiwezi kupiga kura kwenye maazimio ya Baraza Kuu la Umoja huo.Picha: Bebeto Matthews/AP Photo/picture alliance

Nchi zinazotambua mamlaka ya Palestina kama taifa

Nchi 139 kati ya zote 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa hutambua mamlaka ya Wapalestina kuwa taifa.

Soma vilevile: Bendera ya Palestina Yapepea Umoja wa Mataifa

Soma pia: Mashirika ya UN yashinikiza kwa pamoja usitishaji vita Gaza

Maombi ya kutaka kuruhusiwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa ni sharti yaidhinishwe na nchi tisa kati ya 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ikiwa nchi yoyote kati ya tano zenye kura ya turufu ikiwa ni China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani itapinga ombi hilo, basin chi haiwezi ikajumuishwa.

Soma: Palestina kuwasilisha tena azimio la kudai taifa huru

Mamlaka ya Wapalestina haitambuliwi na Marekani, Ufaransa na Uingereza kama taifa.

Mataifa hayo matatu yamesema hayatatambua utaifa wa mamlaka ya Wapalestina hadi mgogoro wao na Israel utakaposuluhishwa.

Msimamo wa Ujerumani kuhusu mamlaka ya palestina

Kama ilivyo nchi nyingi za Umoja wa Ulaya, Ujerumani pia haitambui Palestina kama dola. Hata hivyo inaunga mkono kuundwa kwa taifa la Palestina katika siku zijazo kama sehemu ya suluhisho la mataifa mawili kumaliza mzozo na Israel. Hayo ni kulingana na wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani.

Isreal yasherehekea miaka 70 ya uhuru

01:36

This browser does not support the video element.

Nchi tisa za Umoja wa Ulaya zinatambua utaifa wa mamlaka ya Wapalestina. Lakini karibu nchi hizo zote tisa isipokuwa Sweden, ni zile ambazo wakati mmoja zilikuwa wanachama wa uliokuwa Muungano wa Soviet.

Soma: Rais Abbas atimiza miaka 10 madarakani

Kwa sasa mamlaka ya Wapalestina inachukuliwa kama mshiriki wa Umoja wa Mataifa asiye mwanachama, kumaanisha inakaribishwa kushiriki kwenye vikao vya Baraza Kuu la Umoja huo na inaweza kuendelea kuwa na ofisi zake katika makao makuu ya umoja huo mjini New York.

Kwa sababu ya hadhi yake ya kuwa mshiriki asiye mwanachama iliyotolewa mwaka wa 2012, mamlaka ya Wapalestina ilipewa uanachama katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) mwaka wa 2015, mahakama pekee ya kudumu ya kimataifa inayoweza kuwashtaki watu binafsi kwa uhalifu wa kivita.

Ripoti yake Clare Roth na kutafsriwa John Juma

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW