1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaanza mchakato wa kumrejesha Carles Puidgemont

3 Aprili 2018

Mwendesha mashtaka  mmoja  nchini Ujerumani, ametuma maombi ya waranti wa kurejeshwa Uhispania kwa aliyekuwa rais wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont,ili kushtakiwa kwa makosa ya uasi.

Carles Puigdemont, Ansprache
Picha: Reuters

Mwendesha mashtaka  wa jimbo la kaskazini mwa Ujerumani, Schleswig-Holstein linalopakana na Denmark alitangaza Jumanne baada ya kuwasilisha maombi mbele ya mahakama kuu ya jimbo katika mji wa Schleswig.

Mwendesha mashtaka  huyo amehitimisha, "ombi la kumrejesha Puigdemont kwao lipo, kwamba mchakato mzuri wa kumrejesha unatarajiwa na kuzuiliwa kwake kunahitajika kwasababu ya hatari ya kutoroka,” Kwa mujibu wa taarifa.

Uamuzi huo uliafikiwa kwa misingi kuwa mashtaka anayokabiliwa nayo Puigdemont ni sawa chini ya sheria za Ujerumani, ambazo zinahitaji raia wa Ulaya kukamatwa kwa kutolewa waranti. Alisema kuwa, Puigdemont aliendelea na mpango wake wa kuitisha kura huru ya maoni licha ya kuwa ghasia zilitarajiwa.

Mahakama yasubiriwa kutoa uamuzi

Mahakama kuamua iwapo Puidgemont atarajeshwa UhispaniaPicha: Getty Images/A. Gebert

Mahakama sasa lazima iamue iwapo itatekeleza waranti hiyo ya kumrejesha. Puidgemont kwa sasa yuko kizuizini nchini Ujerumani.

Jumanne msemaji alisema kuwa ombi hilo limepokelewa na tayari lilikuwa linaangaliwa, lakini hakuelezea muda utakaochukuliwa, hata hivyo alisema baada ya siku kadhaa.

Wakili wa Puigdemont Till Dunckel alisema, "timu yangu tayari imeanza harakati za kupinga ombi hilo la kurejeshwa kwake. Mawakili wa upande wa utetezi tayari wamejaza maombi ya kukataa waranti hiyo.” Aliyasema hayo akiwa Hamburg.

Wakili wa Uhispania wa Puigdemont Jaume Alonso-Cuevillas amekiambia kituo cha redio RAC1 kuwa walitarajia ombi la waranti hiyo lakini ana imani kuwa litakataliwa kwasababu ya kukiuka haki za msingi za Puigdemont.

Wakili wa Puigdemont amekata rufaa

Puigdemont alizuiliwa kuingia Ujerumani zaidi ya juma moja alipokuwa akijaribu kurejea kutoka Finland kuelekea Ubelgiji ambapo amekuwa akiishi uhamishoni. Hayo yalitokea baada ya jaji wa Uhispania kutoa waranti ya Ulaya ya kukamatwa kwake.

Polisi wanajaribu kutuliza waandamanaji wa Puigdemont Picha: Getty Images/AFP/R. Roig

Puigdemont amekata rufaa katika mahakama ya Juu ya Uhispania akitaka mashtaka ya uasi na matumizi mabaya ya fedha dhidi yake yatupiliwe mbali.

Katika rufaa ya kurasa 85 iliyonukuliwa na vyombo vya habari vya Uhispania siku ya Jumatatu, Puigdemont ameyakanusha makosa yote mawili akihoji kuwa hakukuwa na ghasia za aina yoyote tarehe mosi, Oktoba wakati kura ya maoni ilipoendeshwa.

Rufaa hiyo iliyotayarishwa na wakili wa upande wa utetezi wa Puigdemont, Jaume Alonso Cuevillas, pia imewasilishwa kwa niaba ya waliokuwa mawaziri wawili wa Catalan, Clara Ponsati na Luis Puig, ambao walitoroka Uhispania baada ya kura hiyo ya maoni.

Kwenye rufaa hiyo wanahoji kuwa raia waliwajibika kwa matendo yao.

Aliyekuwa waziri wa elimu wa Catalan alijisalimisha  katika kituo cha polisi juma lililopita jijini Edinburgh, Scotland.

Wote wanakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 30 iwapo watahukumiwa kwa makosa ya uasi.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Adp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman



 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW