1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Je, Urusi iko imara kiasi gani baada ya uasi wa Wagner?

1 Septemba 2023

Uasi wa Kikundi cha Wagner umefifia ghafla hasa kipindi hiki ambacho kiongozi wake, Yevgeny Prigozhin, amekufa. Lakini matukio ya hivi karibuni yameacha alama yao, Lakini je, Nguvu ya Urusi imo ukingoni ?

Russland Moskau | Präsident Putin leitet Videokonferenz zu wirtschaftlichen Themen im Kreml
Rais wa Urusi Vladmir PutinPicha: Alexander Kazakov/AP Photo/picture alliance

Uasi wa Kikundi cha Wagner umefifia ghafla hasa kipindi hiki ambacho kiongozi wake, Yevgeny Prigozhin, amekufa. Lakini matukio ya hivi karibuni yameacha alama yao. Je, Rais Putin wa Urusi bado ana nguvu kiasi gani?  Je, nguvu ya nyuklia ya Urusi imo ukingoni mwa machafuko? 

Soma zaidi: Ukraine yaushambilia mji wa Urusi kwa droni karibu na kinu cha nyuklia

Wakati maelfu ya mamluki wa Kundi la Wagner walipoandamana kuelekea Moscow miezi miwili iliyopita, walikabiliana na upinzani mdogo kutoka kwa Urusi, Siku iliyofuata, kiongozi wao, Yevgeny Prigozhin, ambaye amekufa katika ajali ya ndege wiki iliyopita, alisitisha mapinduzi hayo, na  hivyo mapambano ya kuwania madaraka yaliyotarajiwa ya Kremlin hayakuweza kufaulu.

Lakini watu hawajasahau jinsi Rais wa Urusi Vladimir Putin alivoonekana akiwa dhaifu wakati alipozungumza kwa mara ya kwanza baada ya tukio hilo ambalo alizungumzia juu ya ''majadiliano'' na kisha "usaliti" uliotokea katika kipindi cha masaa machache.

Tangu kushindwa kwa tukio hilo la uasi, kumekuwa na mjadala kuhusu uimara na utulivu wa serikali ya Urusi. Janis Sarts, mkurugenzi wa Kituo cha Mawasiliano cha kimkakati na ufanisi cha NATO huko Riga, Latvia anaamini maandamano ya Moscow yalikuwa pigo kwa mamlaka ya  Kremlin.

Mwanajeshi wa kundi la Wagner akiweka maua kufuatia kifo cha kiongozi wao Yevgeny PrigoschinPicha: Maxim Shemetov/REUTERS

Na naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Masuala ya Kimataifa huko Latvia Martins Vargulis anaamini kuna mvutano wa kijeshi ndani ya Urusi unaotishia mamlaka ya Rais Putin.

Soma zaidi: Wanajeshi sita wa Ukraine wauwa katika ajali ya ndege

Wakati huo huo, mfumuko wa bei nchini Urusi unaendelea kuongezeka, huku fedha ya Urusi Ruble ikiendelea kudorora dhidi ya dola na euro. Mamlaka mjini Moscow zinakiri kuwepo kwa misururu mirefu katika vituo vya mafuta nchini Urusi, sehemu ambayo ndiyo mzalishaji mkubwa wa mafuta nambari tatu duniani.

Vita vya Urusi nchini Ukraine vinaonesha kuyumba kwa sasa, na kwa wiki za hivi karibuni  Ukraine  ndiyo imekuwa ikiripoti kupiga hatua zaidi katika uwanja wa vita.

 Je, Rais Putin anapoteza nguvu aliyonayo ya kimamlaka?.

Stefan Meister wa Baraza la Ujerumani la Mahusiano ya Kigeni (DGAP) anakiri kwamba bado Putin anayo nguvu. Ameiambia DW kwamba utawala wa Putin umeweza kushinda sehemu kubwa ya watu kwa ukandamizaji na propaganda na unasimamia kukwepa vikwazo vya Magharibi kwa kiwango fulani. Kampuni nyingi, pamoja na zingine za Magharibi, bado zinafanya kazi nchini Urusi.

Meister anasema ni kweli kumepungua kwa ustawi miongoni mwa raia wa  Urusi, lakini nchi hiyo haiwezi kusemwa kuwa inasambaratika, wala Putin haonyeshi dalili za udhaifu.

Wanajeshi wa kundi la mamluki la WagnerPicha: REUTERS

Anaamini kwamba kama Putin atashambuliwa siku moja, basi huyo mtu atakuwa ametokea ndani ya vyombo vyake vya usalama.  Ingawa, mtaalam huyo wa Urusi anaamini kwamba Putin bado  ana rasilimali za kutosha kuendeleza vita vyake dhidi ya Ukraine kwa miaka mingine miwili au mitatu.

Hali ya Putin kijeshi iko vipi kwa sasa?

Tobias Fella, Mtafiti katika Taasisi ya Utafiti wa Amani na Sera ya Usalama (IFSH), anasema kwamba Urusi kwa sasa bado iko imara na haikabiliwi na tishio lolote. Hata hivyo, Bado kuna matatizo machache ndani ya Kremlin ikiwa serikali italazimika kuhamasisha wanajeshi zaidi . Fella anatoa maoni kwamba Urusi imejidhihirisha kuwa kama kinyonga anayejibadilisha kila wakati katika mapambano yake dhidi ya Ukraine.


''Ndio ana makamanda na jambo moja kuu kwa Putin ni kwamba anathamini sana wanajeshi watiifu kuliko wale ambao wanatajwa kuwa ni wajuzi , kwa sababu hataki watu ambao wanaweza kukinzana na amri zake kwa jeshi na yale anayotaka kuyatelekeza kwa namna yake'' amesema Tobias Fella.

Nani anaweza kumdhibiti Putin?

Wachambuzi wa nchi za Magharibi wanakisia kwamba Kremlin yenyewe inaweza kuwa inaeneza simulizi kwamba Urusi inaelekea ukingoni mwa machafuko. Kama hali ingekuwa hivyo, wanapendekeza, lengo lingekuwa kudhoofisha uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa Ukraine - wazo likiwa ni kwamba nchi za Magharibi zinaweza kukubali Ukraine kulazimishwa kuacha eneo lakini sio makombora ya nyuklia ya Urusi.

Kwa mujibu wa Meister,anasema kushindwa kijeshi kwa Urusi katika maeneo machache nchini Ukraine haimaaniishi kuwa Putin hana nguvu za kutosha na haimuweki hatarini. Kitu pekee kinachoweza kuleta mabadiliko ni ikiwa Ukraine itafanikiwa kurudisha katika himaya yake jimbo la Crimea na maeneo yake yote yanayokaliwa kwa sasa na Urusi.


 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW