1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Je Scotland itaruhusiwa kuandaa kura ya kujitenga?

23 Novemba 2022

Mahakama ya juu kabisa ya Uingereza itaamua ama kuipa mamlaka serikali ya Scotland kuandaa kura ya maoni kuhusu kujitenga au kuyabakisha mamlaka hayo London

Schottland | Nicola Sturgeon
Picha: Jane Barlow/PA Wire/empics/picture alliance

Mahakama ya juu kabisa nchini Uingereza inatarajiwa kutoa uamuzi leo Jumatano ikiwa Scotland inaweza kuendesha mchakato wa kura ya maoni kuhusu kujitenga bila ya kuitaka ridhaa serikali ya mjini London, kesi ambayo inaweza kuwa na athari kubwa kwa mustakabali wa baadae wa Uingereza.

Scotland yenye mamlaka yake ya ndani lakini ikiwa ni sehemu ya Uingereza imeitaka mahakama hiyo ya juu ya Uingereza kuamua ikiwa bunge la Scotland linaweza kupitisha sheria ya kuandaa kura ya maoni kuhusu kujitenga Oktoba mwaka ujao.

Serikali ya Uingereza mjini London inayoongozwa na chama cha wahafidhina haitaki kuidhinisha mchakato huo wa kura ya maoni ya Scotland, ikisema suala hilo lilishamalizika katika kura ya maoni ya mwaka 2014 ambayo ilishuhudia Wapiga kura wascotland wakipitisha uamuzi wa kukataa kujitenga na Uingereza.

Picha: Danny Lawson/PA Wire/picture alliance

Asilimia 55 ya wananchi wa Scotland walipiga kura ya hapana wakati 45 waliunga mkono kujitenga na Uingereza.

Mtamazo Scotland

Hata hivyo hivi sasa serikali ya Scotland iliyoko mjini Edinburgh ambayo inapigia upatu hatua ya kujitenga inataka suala hilo litazamwe tena, kwa kutoa hoja kwamba kujiondowa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya , kumeibadili kwa kiasi kikubwa mitizamo ya kisiasa na kiuchumi miongoni mwa WaScotland ambao kimsingi wengi hawakuunga mkono Uingereza kujiondowa Umoja wa Ulaya.

Waziri Kiongozi wa Scotland Nicola Sturgeon, amehoji kwamba anamamlaka ya kidemokrasia kutoka kwa wananchi wake kuitisha mchakato wa kura ya kutaka kujitenga kwa sababu sehemu kubwa ya bunge la Scoltand wanaunga mkono kujitenga.

Itakumbukwa kwamba katika kikao cha mahakama ya juu kilichofanyika mwezi uliopita afisa wa ngazi ya juu kuhusu masuala ya sheria katika serikali ya Scotland, Dorothy Bain alisema wabunge wengi katika bunge la Edinburgh walipigiwa kura na wananchi kuingia bungeni kwa ahadi ya kuwa tayari kuitisha kura ya maoni ya kujitenga na Uingereza.

Lakini pia aliweka wazi kwamba kura ya maoni itakuwa kama mchakato wa kutowa mapendekezo na wala haitokuwa ni haitokuwa inalazimisha kisheria, ingawa pia ikiwa Wascotland wataamua kuunga mkono kujitenga kwa kupiga kura ya ndio, basi ni jambo litakaloongeza chachu kwa Scotland kujitenga.

Pamoja na hayo kwa upande wa London mwanasheria wa serikali ya Uingereza James Eadie anasisitiza kwamba mamlaka ya kuitisha kura ya maoni yanabakia kwenye bunge la Uingereza mjini London kwasababu ya umuhimu wake kwa nchi nzima ya Uingereza kwa ujumla wake na sio tu kwa Scotland.

Picha: Jeff Mitchell/Getty Images

Uchunguzi wa maoni

Kwahakika uchunguzi wa maoni unaonesha kwamba Wascotland wamegawika nusu kwa nusu katika suala hili la kujitenga na pia wapiga kura waliowengi hawataki kura nyingine ya maoni kwa hivi karibuni.

Kinachosubiriwa katika mahakama ya juu ni uamuzi wa  Majaji watano wa mahakama hiyo ambao huenda wakapitisha uamuzi kwamba Scotland inayo mamlaka ya kuitisha kura ya maoni,au wakasema haina mamlaka hayo au wanaweza wakakataa kutoa uamuzi kabisa.

Ingawa vilevile kwa upande mwingine mtaalamu wa masuala ya kisheria kutoka Scotland Andrew Tickell anasema hata ikiwa serikali ya Scotland itapata ushindi kwenye kesi hii na kupata fursa ya kupitisha sheria ya kuitisha kura hiyo ya maoni, hautokuwa mwisho wa suala hili.

Inaelezwa kwamba wanaounga mkono kujitenga wanapanga kuandamana nje ya bunge la Scotland mjini Edinburgh na katika maeneo mengine baada ya kutangazwa uamuzi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW