1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiUjerumani

Je, ukomo wa deni la Ujerumani ni nini hasa?

30 Novemba 2023

Kutokana na hukumu wa Mahakama ya Katiba, bajeti ya Ujerumani kwa mwaka huu ina nakisi ya euro bilioni 60. Lakini katiba ya nchi hiyo inazuwia hatua yoyote ya kuziba pengo hilo kwa kuchukuwa mikopo mipya,

Schuldenuhr Deutschlands I Berlin
Picha: Daniel Kalker/dpa/picture alliance

Nchini Ujerumani, serikali ya shirikisho na majimbo 16 ya shirikisho yanalazimika kusawazisha hesabu zao, na yamepigwa marufuku kuchukua mikopo ya ziada. Hakuna nchi nyingine ya G7 iliyo na vikwazo vikali kama hivyo vya kuchukua mikopo ya ziada. Sheria zimewekwa katika Sheria ya Msingi, yaani katiba ya Ujerumani, na zinatumika - pamoja na tofauti ndogo - katika ngazi ya shirikisho na katika majimbo 16, yanayojulikana kama Länder.

Kifungu cha 109 cha Sheria ya Msingi, aya ya 3, kinasema: "Bajeti za Shirikisho na Majimbo, kimsingi, zitasawazishwa bila mapato yatokanayo na mikopo." Hii inamaanisha kuwa serikali inaweza tu kutumia pesa kiasa sawa na ilivyokusanya, hasa kutokana makusanyo ya kodi na ushuru. Sharti hili linajulikana kama "breki ya deni."

Kuokoa vizazi vijavyo

Sheia hiyo ilianzishwa mwaka wa 2009 chini ya Kansela Angela Merkel, wa chama cha Christian Democratic Union, CDU, na Waziri wake wa Fedha Peer Steinbrück, wa chama cha Social Democratic, SPD. Ilianzishwa katikati ya msukosuko wa kifedha na kiuchumi duniani ambapo kulikuwa na mijadala mingi kuhusu deni la taifa.

Angela Merkel na waziri wake wa fedha Peer Steinbrück walianzisha kanuni ya ukomo wa deni mwaka 2009.Picha: picture-alliance/ dpa

Katika hotuba kwa mawaziri wakuu wa serikali wakati huo, Steinbrück alizungumzia "uamuzi wenye umuhimu wa kihistoria - uamuzi ambao unapaswa kudhamini uwezo wa kifedha wa serikali kuchukua hatua, hasa kuhusu haki kati ya vizazi."

Soma pia: Scholz: Tutafanya juu chini kutatua mzozo wa bajeti

Lakini mjadala wa kisiasa wenye utata ulizingira utangulizi huo. Chama cha Kijani (wakati huo kilikuwa cha upinzani) na Chama cha mrengo mkali wa kushoto, Die LInke,  vilikuwa vikipinga vikali, vikisema kwamba serikali ilikuwa inazuia uwezo wake wa kutenda.

Watetezi wa breki ya deni, kwa upande mwingine, walisema kwamba serikali italazimika kutumia pesa zaidi na zaidi kwa riba kadiri mlima wa deni unavyokua. Hii, walisema, itakuwa kikwazo zaidi na mzigo kwa vizazi vya watu.

Bajeti zasawazishwa kuanzia 2014 hadi 2019

Ukomo wa deni ulianza kuwa nan nguvu ya kisheria kwa serikali ya shirikisho mnamo mwaka 2016 na kwa majimbo mwaka 2020. Hata hivyo, mnamo 2014, Waziri wa Fedha wa Shirikisho la wakati huo Wolfgang Schäuble (CDU) tayari alikuwa na uwezo wa kuwasilisha bajeti iliyosawazishwa kwa mara ya kwanza katika miaka 45. Neno "sifuri nyeusi" lilibuniwa kuashiria mafanikio ya Schäuble, na likawa kauli mbiu ya kisiasa, kwa sababu matumizi na mapato viliwiana.

Hata hivyo sheria ya breki ya deni siyo jambo lisiloweza kubadilishwa, angalau sio kwa serikali ya shirikisho. Ingawa marufuku ya moja kwa moja ya deni inatumika kwa majimbo ya shirikisho, serikali ya shirikisho inaruhusiwa kukopa kwa jumla kwa kiwango cha juu cha asilimia 0.35 ya uzalishaji wa kiuchumi. Mfano: Pato la jumla la ndani la Ujerumani lilifikia takriban euro trilioni 3.88 trilioni mwaka 2022, kumaanisha kuwa serikali ya shirikisho ingeruhusiwa kuchukua takriban euro bilioni 13 katika deni la ziada.

Washirika wa serikali ya muungano ya Ujerumani, Kansela Olaf Scholz, kulia, kutoka SPD, Robert Habeck, kutoka chama cha Kijani, katikati, na Christian Lindner, FDP.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Virusi vya Corona na vita vya Ukraine

Hata hivyo, serikali ilikopa mahali fulani katika kiwango cha euro bilioni tatu mnamo 2022. Hiyo ni kwa sababu bunge la Ujerumani, Bundestag, lilipiga kura kutumia kuweka kando sheria ya ukomo wa deni, kama lilivyokuwa tayari limefanya kwa 2020 na 2021: Ikirejelea matokeo ya janga la virusi vya na vita nchini Ukraine, bunge lilidai "hali ya dharura isiyo ya kawaida."

Soma pia: Rungu la Mahakama latikisa sehemu ya bajeti ya Ujerumani

Sheria ya Msingi inaruhusu breki ya deni kusitishwa "kazika mazhingira ya majanga ya asili au hali zisizo za kawaida za dharura nje ya udhibiti wa serikali na zinazodhuru kwa kiasi kikubwa uwezo wa kifedha wa serikali." Katika mjadala wa sasa wa bajeti ya 2024, chama tawala cha SPD na Kijani kwa mara nyingine tena vinataka hali ya dharura itangazwe kwa misingi ya matokeo ya kifedha ya vita vya Ukraine na mzozo wa nishati utokanao na vita hivyo.

Je, sheria ya ukomo wa deni ni kali sana?

Wakati huo huo, mjadala umezuka juu ya iwapo breki ya deni inapaswa kurekebishwa. Baadhi ya wanauchumi wanaunga mkono hili, wakisema sheria hiyo inatatiza uwezo wa serikali kuwekeza katika miundombinu na teknolojia za siku za usoni.

Hata hivyo, mageuzi ya breki ya deni hayawezekani kwa muda mfupi kwa sababu Sheria ya Msingi inaweza tu kurekebishwa kwa kura ya thuluthi mbili katika Bundestag. Wingi huu haupo kwa sasa kwa sababu vyama vya kihafidhina vya CDU na CSU, ambavyo kwa pamoja vinaunda kundi kubwa la wabunge wa upinzani, vinapinga marekebisho hayo.