1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, unawezaje kutambua propaganda za serikali?

7 Januari 2022

Wanasiasa ulimwenguni kote huwachezea watu ili kuathiri mawazo na matendo yao. Na hii hutokea kote kote. Lakini ninawezaje kutambua propaganda za serikali? Timu ya kuchunguza ukweli ya DW inatoa vidokezo.

Belarus TV Ansprache Lukaschenko
Picha: Sergei Grits/AP Photo/picture alliance

Hila za serikali ya Ufilipino zinachukuliwa kama ushahidi tosha wa propaganda za serikali - alau tangu mwanahabari Maria Ressa alipopokea Tuzo ya Amani ya Nobel kuhusiana na mapambano yake dhidi ya propaganda na uwongo wa serikali.

Propaganda za serikali pia zina makao katika demokrasia nyingine na katika ulimwengu wa Magharibi. Mfano nchini Marekani, namna serikali ilivyouza vita vya Iraq kwa raia.

Propaganda si jambo geni - lakini kwa sasa imefikia mwelekeo mpya. Chini ya Ujamaa wa Kitaifa, njia za propaganda zilitumiwa waziwazi kuwashawishi watu juu ya itikadi ya mtu mwenyewe.

Leo, propaganda mara nyingi hufanyika kwa njia iliyofichika zaidi - mara nyingi kupitia mnjia mpya za upashaji habari kama vile mitandao ya kijamii.

Mifano michache: Hivi karibuni zaidi, kampuni ya Meta (zamani Facebook) ilifuta kampeni kubwa ya upotoshaji iliyokuwa inaendeshwa na serikali Nikaragua, kulingana na taarifa za kampuni hiyo.

Kwenye tovuti na kupitia akaunti mbalimbali za mitandao ya kijamii, Rais Daniel Ortega alikuwa akishangiliwa kwa zaidi ya miaka mitatu - na upinzani ukitiwa fedheha.

Picha: Alexander Limbach/Zoonar/picture alliance

Mfano mwingine: Mnamo Septemba, chaneli mbili za Youtube za shirika la habari la Russia Today nchini Ujerumani, zilifungiwa kwa kueneza habari potofu kuhusu virusi vya corona.

Idhaa hiyo ya kimataifa ya serikali ya Urusi hii leo inachukuliwa kama chombo cha kueneza propaganda za serikali ya Urusi. Kulingana na wasomi wawili wa Chuo Kikuu cha Oxford, ajenda kuu ya idhaa hiyo ni kueneza kwamba vyombo vya habari vya Magharibi vinadanganya.

Lakini propaganda ni nini? Na jinsi ya kuitambua? Nakala hii inatoa majibu kwa maswali haya. Ili kufanya hivyo, tulizungumza na wataalam wanne.

Propaganda ni nini?

Wanasiasa hutumia propaganda hasa kushawishi mawazo, matendo na hisia za watu. Watu wanashawishiwa kuchukua mtazamo au msimamo kwa njia ya ujanja, anaeleza Piers Robinson, mwanasayansi wa siasa kutoka Shirika la Mafunzo ya Uenezi, katika mahojiano ya DW.
 

"Kwa mfano, kisa maarufu cha Iraq mwaka 2003. Unajaribu kuwashawishi watu waunge mkono uvamizi wa Iraq, hivyo unawaaminisha kwamba kuna kitisho kinasababishwa na Iraq na bila shaka katika kisa hicho maarufu, walitia chumvi taarifa za intelijensia kuhusu silaha za maangamizi makubwa na kuifanya Iraq ionekane kitisho kikubwa zaidi kuliko uhalisia," alisema Robinson.

Mtafiti wa habari Florian Zollmann kutoka Chuo Kikuu cha Sanaa na Utamaduni mjini Newcastle Uingereza, pia anatoa mfano wa Marekani na Iraq katika mahojiano na DW. "Habari potofu na habari za uwongo ni sehemu ya propaganda", Zollmann anasema. "Kwa hivyo huwezi kutenganisha wazi madai ya uwongo na propaganda."

Kulingana na Robinson na Zollmann, fani ya mahusiano ya umma haipaswi pia kupuuzwa. "Mwisho wa siku, hizi zote ni mbinu za propaganda," Zollmann anaelezea. "Hiyo haimaanishi kwamba propaganda daima ni mbaya," anafafanua na kuongeza kuwa  unapaswa kufahamu kwamba watu pia wanapaswa kuathiriwa na mahusiano ya umma.

Ni lipi lengo la propaganda za kisiasa?

"Lengo kuu ni kujenga taswira nzuri ya wanasiasa na serikali," anasema Pavel Koshkin, mtafiti katika Taasisi ya Mafunzo ya Marekani na Kanada katika Chuo cha Sayansi cha Urusi na mhariri mkuu wa zamani wa jukwaa la mtandaoni la Urusi la Russia Direct. . Huko Urusi, propaganda za serikali hutumiwa kuunda picha ya demokrasia ya Urusi.

Propaganda za kisiasa wakati mwingine sio tu zinalenga kuchora taswira nzuri ya nchi yako - lakini pia kuweka nchi, tamaduni au maadili katika mtazamo mbaya. Kwa mfano, utafiti wa Wakfu wa Maendeleo ya Vyombo vya Habari unaonyesha jinsi propaganda dhidi ya Magharibi inavyoenezwa katika vyombo vya habari vya Georgia.

Mtaalamu wa mawasiliano Robinson anasisitiza, hata hivyo, kwamba propaganda haifanywi tu katika nchi kama Urusi, China au Korea Kaskazini. "Nadhani tatizo katika nchi za kidemokrasia ni kwamba kuna propaganda nyingi lakini hatujui," alisema Robinson.

"Kwa hakika tuna propaganda nchini Ujerumani na Marekani pia," anaeleza mwenzake Zollmann. Propaganda inatumika katika nchi za kiimla na za kidemokrasia. Tofauti ya propaganda katika udikteta, hata hivyo, katika demokrasia upatikanaji wa habari kutoka kwa vyombo vingine vya habari ni rahisi zaidi.

Lipi jukumu la vyombo vya habari katika kueneza propaganda za kisiasa?

Kwa upande mmoja, vyombo vya habari vinaweza kuwasilisha na kuimarisha propaganda, anasema Christian Mihr wa shirika la Waandishi Habari wasio na Mipaka katika mahojiano na DW.

Kwa mfano, kituo cha televisheni cha Russia Today kinakosolewa mara nyingi kwa kuwa chombo cha propaganda cha Kremlin.

Russia Today inafadhiliwa na serikali mjini Moscow na "inaonyesha hasa maoni rasmi ya serikali ya Urusi," yasema tovuti ya Shirika la Shirikisho la Elimu ya Kiraia.

Hata kituo cha utangazaji cha Poland TVP pia kinashutumiwa mara kwa mara kwa kutumia mbinu za propaganda na kukitukuza chama tawala cha PiS.

Vyombo vya habari vinaweza kusambaza propaganda kwa uangalifu, lakini pia bila kujua. Ili kufichua propaganda, vyombo vya habari vinapaswa kutenda kama "walinzi", anasema mwanasayansi wa propaganda Robinson.

Hilo ndilo watu wangetarajia - na kulingana na utafiti wa vyombo vya habari, ni mojawapo ya kazi kuu za uandishi wa habari.

Bora zaidi, waandishi wa habari wanaweza kuainisha propaganda za kisiasa, anasema Mihr wa Shirika la Waandishi Wasio na Mipaka.

Kwa mfano, kuuliza wanasiasa maswali muhimu na kuuliza wataalam wa kujitegemea juu ya mada. Propaganda za kisiasa mara nyingi hufichwa, lakini inawezekana kuziona.

Chanzo: DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW