1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, wingi wa von der Leyen EU unatosha kumpa mhula wa pili?

17 Julai 2024

Kura ya siri ya Bunge la Ulaya itaamua kama Ursula von der Leyen atahudumu kwa muhula wa pili kama rais wa Tume ya Ulaya. "Itakuwa ngumu," mtaalamu mmoja aliiambia DW.

Belgium, Brussels | Rais wa Halamshauri Kuu ya Umoja wa Ulaya | Ursula von der Leyen
Hotuba ya von der Leyen siku ya Alhamis itaamua iwapo wabunge watamuunga mkono kuogoza mhula wa pili.Picha: Dursun Aydemir/Anadolu/picture alliance

Ursula von der Leyen alishinda nusu tu ya mapambano wakati viongozi wa Umoja wa Ulaya walipomuidhinisha kwa muhula wa pili kama rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya mwezi Juni.

Sasa, bado anahitaji kushawishi idadi kubwa zaidi wabunge 720 wa Bunge la Ulaya siku ya Alhamisi.

Von der Leyen atajinadi kama kiongozi mwenye uzoefu na huenda akanufaika kutokana na shauku ya miji mikuu ya Ulaya kuwa na kiongozi thabiti katika wakati ambapo vita vinarindima nchini Ukraine na hofu ya uwezekano wa Donald Trump kurudi madarakani nchini Marekani, kutikisa ushirikiano wa kimataifa.

Kundi la kisiasa la Von der Leyen, la European People's Party, EPP, lina viti 188, Wasoshalisti na Waliberali wana viti 136, na kundi la kiliberali la Renew lina viti 77. Idadi hii ni kubwa zaidi kuliko kura 361 anazohitji kushinda mhula wa pili.

Soma pia:Umoja wa Ulaya kuwaidhinisha viongozi wakuu wa taasisi hiyo 

Kwenye karatasi, inaweza kuonekana kuwa rahisi kwake kukusanya kura zinazohitajika kutoka ndani ya muungano huo.

"Mimi si mtaalamu wa hisabati, lakini nadhani kwa nguvu ya makundi matatu ya mrengo wa kati yanayomuunga mkono Ursula von der Leyen na yanayounda sehemu ya mpango wa makubaliano, tunazo takwimu," msemaji wa EPP Pedro Lopez alisema wiki iliyopita.

Lakini wanasiasa na wachambuzi waliozungumza na DW wanaamini kitakuwa kinyang'anyiro kigumu. "Itakuwa ngumu," alisema Julien Hoez, mtaalam wa EU mwenye makao yake makuu mjini Brussels.

Kura zinapigwa kwa siri

Kwa kuwa kura hiyo itakuwa ya siri, ni muhimu kwa von der Leyen kuzungumza binafsi na wabunge, wanaoweza kupiga kura kulingana na maslahi ya waliowachagua bila kuhofia madhara ikiwa watajitenga na msimamo wa vyama vyao.

Na wakati wabunge wa Uaya hawalazimiki kumpigia kura mgombea kupitia mnadhimu wa chama, serikali na viongozi bado wanaweza kushawishi matokeo.

Kura ya siri inamaanisha hakuna hatua za adhabu kwa wabunge wanaochagua kinyume na msimamo wa vyama.Picha: Ramon van Flymen/EPA

Waziri Mkuu wa Ireland Simon Harris, kwa mfano, ametoa wito kwa MEPs wa Ireland kumuunga mkono von der Leyen kwa nia ya kupata wadhifa muhimu wa Tume ya Ulaya kwa Ireland. Tume hiyo yenye wanachama 27 ina kamishna kutoka kila nchi wanachama, na baadhi ya nyadhifa zina ushawishi zaidi kuliko nyingine.

"Sina shaka kwamba Rais von der Leyen atataka kuzungumza na MEPs. Hilo litakuwa jambo linalofaa kufanya, na, kwa hakika, nitakuwa nikishirikiana na MEPs wa Ireland kwa msingi kwamba sasa tumempendekeza Michael McGrath kuwa kamishna wetu," alisema Harris, kulingana na shirika la utangazaji wa umma la Ireland RTE.

Soma pia: Uchaguzi wa bunge la Ulaya waanza Uholanzi

Iwapo von der Leyen atashindwa kupata kura 361, Umoja wa Ulaya unaweza unaweza kutumbukia katika mgogoro wakati ambapo wasiwasi ni mkubwa na wagombea mbadala wenye uungwaji mkono wa kutosha wanaonekana kutokuwepo.

Je, von der Leyen atatafuta uungwaji mkono mrengo mkali wa kulia?

Mnamo mwaka 2019, von der Leyen alipita kwa tofauti ndogo sana ya kura 9 akiwa na muungano huo huo.

Safari hii wanasiasa kadhaa ndani ya muungano huo wa vyama vingi tayari wamesema hawatampigia kura, na wengine wameonya kwamba lazima ajiepushe na kushirikiana na kundi la mrengo mkali wa kulia la Conservatives and Reformists (ECR) - kundi la nne kwa ukubwa katika Bunge la Ulaya.

Chama cha von der Leyen cha EPP kimesema hakuna makubaliano rasmi na chama cha Giorgia Meloni cha ECR.Picha: YARA NARDI/REUTERS

Wanasoshalisti na Waliberali wanamtazama von der Leyen kwa karibu kufuatia ukaribu wake kwa Waziri Mkuu wa Italia Georgia Meloni, ambaye anaongoza kundi la ECR.

Kabla ya uchaguzi wa Ulaya mwezi uliopita, von der Leyen alifungua mlango wa muungano na Meloni. Hatua hiyo iliwakasirisha washirika wake wakuu, ambao walitishia kuondoa uungwaji mkono wao ikiwa angeegemea zaidi upande wa kulia.

Soma pia: Utafiti: Wajerumani wachache kujitokeza uchaguzi wa Ulaya

Baada ya uchaguzi, EPP iliashiria kuwa hakutakuwa na makubaliano rasmi na Meloni, lakini kuna nafasi von der Leyen ataipatia Italia makubaliano kuhusu sera ya uhamiaji katika hotuba yake siku ya Alhamisi. Maneno ya ahadi yoyote kama hiyo, na kwa muktadha huo kuhusu mzozo unaoendelea wa Gaza, yatafuatiliwa na Wasoshalisti, Waliberali na Watetezi wa Mazingira.

Watetezi wa Mazingira kuokoa jahazi?

Chama cha Kijani kilipoteza viti 17 katika uchaguzi wa Ulaya wa Juni, lakini hata kwa idadi iliyopungua ya viti 53, wanaamini kuwa wako tayari kuchukua jukumu muhimu katika bunge la EU na kushikilia ufunguo wa kurejea kwa von der Leyen. Kundi hilo linaweza kutoa kura anazohitaji von der Leyen bila yeye kufanya muafaka na Meloni na kuendeleza usawa kati ya mrengo wa kati-kulia na wa kati-kushoto na wanamageuzi.

DW imearifiwa kuwa von der Leyen imewahakikishia wanachama wa chama cha Kijani kuwa amedhamiria kufuata lengo la kuondokana na utoaji kabisa wa hewa chafu ifikapo mwaka 2050 lililowekwa kwenye Mkataba wa vyama vya Kijani vya Ulaya, lakini akaongeza kuwa mpango huo unaweza kuhitaji marekebisho.

Fahamu kuhusu uchaguzi wa Bunge la Ulaya

01:24

This browser does not support the video element.

Von der Leyen atalazimika kuchukuwa tahadhari kubwa kuhusu namna anavyodhamiria kusuluhisha mzozo wa utumiaji wa injini za mwako baada ya 2035. Wakati kundi la EPP, ambalo linahusisha zaidi chama cha Christian Democrats cha Ujerumani, linataka kubatilisha marufuku hiyo, Wanasoshalisti na Kijani wanataka iendelezwe.

Soma pia: Scholz amuonya von der Leyen kutoshirikiana na vyama vya itikadi kali

Wabunge wa Kijani wana uwezekano wa kumpigia kura von der Leyen, na, kama kambi, watamsaidia kuvuka mstari wa mwisho. Wataalamu walisema chama cha Kijani kimekuwa kisikivu zaidi baada ya hasara katika uchaguzi na hakitafuti zaidi ya uhakikisho mpana juu ya kuendelea kwa Mpango wa Kijani.

"Kama kuna mstari mwekundu, basi ni kuufungia nje mrengo mkali wa kulia," alisema mwanasiasa wa Kijani, aliezungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

Von der Leyen atalazimika kusawazisha maslahi tofauti ili kuchaguliwa tena. Mwanasiasa mmoja wa Umoja wa Ulaya aliiambia DW kwamba hawezi kuwashawishi washirika ikiwa analenga tu kutumikia maslahi ya kundi lake la kisiasa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW