1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, kuna kitisho cha kuvurugika hali ya usalama Zanzibar?

6 Oktoba 2025

Wagombea urais Visiwani Zanzibar Hussein Ali Mwinyi (CCM) na mpinzani wake mkubwa Othman Masoud Othman wa chama cha ACT-Wazalendo wamelaumiana juu ya uwezekano wa kuvurugika usalama kuelekea uchaguzi mkuu.

Tanzania | Mgombea urais | Chama cha CCM | Hussein Ali Mwinyi
Mgombea wa urais Visiwani Zanzibar Hussein Mwinyi akiwa kwenye mkutano wa kampeni za urais Picha: Najjat Omar/DW

Siku ya Jumapili Rais Mwinyi anayewania muhula wa pili madarakani aliwaambia viongozi wa dini kwenye eneo hilo ambalo ni ngome kuu ya hasimu wake, Othman Masoud kwamba amejitahidi kwenye kipindi cha mwanzo cha utawala wake kuimarisha amani na kuondosha ubaguzi lakini anasikitishwa na namna wapinzani wanavyosahau kazi kubwa aliyoifanya kwa kumtuhumu kuirejesha nchi nyuma.

"Serikali ya Chama cha Mapinduzi inazungumzia umoja na ndio maana leo hatubaguani. Hapa hapa Pemba, kulikuwa na wakati, misikitini tulikuwa hatusali sote. Huu msikiti bwana wa CCM.... huu msikiti wa CUF... Hapa... Tumesahau? Tulikuwa hatuzikani. Watu walikuwa wanapeana talaka kipindi hiki cha uchaguzi. Tusisahau."

Masoud aonya dhidi ya kurudia kwa matukio ya nyuma

Kauli hiyo ya Rais Mwinyi imetanguliwa na onyo alilolitowa mgombea mkuu wa upinzani Othman Masoud, akiwa hukohuko Pemba siku ya Jumamosi aliyemtumia ujumbe wa wazi Rais Samia Suluhu Hassan kumtaka azuie kile alichosema ni uwezekano wa kurejea kwa matukio ya mwaka 2020.

"Ninachomuomba Rais Samia nayasema hapa. Waliyoyafanya 2020, wakawapa watu ushindi wa wizi, baada ya kuuwa watu, kujeruhi watu, hao waliopewa ushindi wa wizi, umewatamukia. Wameanza kuamini wao wenyewe kwamba eti walishinda 2020. Hao waliowapa ushindi, leo wanafanya mbinu wapate viti walivyopata 2020 kwa namna yoyote."

Watu 20 waliuawa kwenye uchaguzi wa 2020

Katika uchaguzi wa mwaka 2020, zaidi ya watu 20 waliuawa na wengine mamia kujeruhiwa visiwani Zanzibar lakini wengi wao walikuwa ni wa kisiwani Pemba, kwa mujibu wa ripoti za mashirika ya haki za binaadamu.

Matukio ya uchaguzi huo si pekee kwenye historia ya miaka 30 ya chaguzi za vyama vingivisiwani Zanzibar. Kumetokea visa kadhaa vinavyohusishwa moja kwa moja na siasa za uchaguzi, yakiwemo ya kushambuliwa wananchi kwenye mitaa, vijiji na maskani zao na makundi ya vijana, ambayo hapa visiwani yamepewa jina "Masoksi ama Mazombi." 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW