1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, utawala wa mabavu hatarini Tunisia?

13 Januari 2011

Machafuko yanayozidi kushika kasi nchini Tunisia yanautikisa msingi wa serikali ya mabavu inayoongozwa na Rais Zine el Abidine Ben Ali.Je,serikali yake kweli ipo hatarini?

Tunisian President Zine El Abidine Ben Ali waves as he arrives to a meeting marking the 21st anniversary of his access to power,in Tunis, Friday Nov. 7, 2008. (AP Photo/Hassene Dridi)
Rais Zine el Abidine Ben Ali wa TunisiaPicha: AP

Tangu wiki kadhaa,raia wa Tunisia na hasa vijana wanaandamana kulalamika kuhusu ukosefu mkubwa wa ajira, rushwa na jinsi utajiri wa nchi unavyonufaisha wachache nchini humo.Maandamano yaliyofanyika kupinga hali ngumu ya maisha sasa yanazidi kuwa vuguvugu la umma dhidi ya serikali ili kupinga ukandamizaji wa kisiasa nchini humo.

Kila kukicha hali inazidi kuwa mbaya.Ripoti mpya za vifo zimekuwa zikiripotiwa kutoka miji ya ndani na machafuko hayo sasa yamefika katika mji mkuu Tunis.Kufuatia mapambano makali yaliyozuka hiyo jana kati ya polisi na waandamanaji, watu hawaruhusiwi kutoka nje wakati wa usiku na wanajeshi wanapiga doria barabarani.

Wanajeshi wanapiga doria katika mji mkuu TunisPicha: picture alliance / dpa

Maandamano hayo ya vijana ni changamoto kali kwa serikali ya Rais Zine el Abidine Ben Ali, anaetawala kwa mabavu tangu kushika madaraka miaka 23 iliyopita huku makundi ya upinzani yakikandamizwa.Licha ya machafuko hayo,wachambuzi wa kisiasa hawaamini kuwa ghasia hizo zitaweza kuhatarisha mfumo wa serikali yake ya mabavu. Mtaalamu wa masuala ya eneo la Maghreb, Hardy Ostry wa taasisi ya Konrad Adenauer anaeleza hivi:

"Kwa maoni yangu ni mapema mno kudhania kuwa huu ni mwisho wa serikali ya Ben Ali - hasa kwa kulinganisha matukio mengine yaliyowahi kushuhudiwa nchini Tunisia na nchi zingine katika kanda hiyo."

Waandamanaji wakimshinikiza Rais Zine el Abidine Ben Ali kuondoka madarakaniPicha: AP

Kwa upande mwingine,katika maandamano ya sasa imedhihirika kuwa hakuna alieshika usukani.Waandamanaji wanawasiliana kwa simu za mkono na mtandao, lakini hawana mwongozo maalum wala shirika lolote lile la kuwaongoza. Ghasia hizo,ziliendelea jana usiku na milio ya risasi ya hapa na pale ilisikika nje ya mji mkuu. Hiyo,licha ya kutangazwa amri ya kutotoka nje wakati wa usiku katika jitahada ya kutuliza ghasia hizo. Kwa mujibu wa ripoti ya mashahidi wawili,katika mapambano na polisi, mwanamume wa miaka 25 ameuawa ukingoni mwa mji mkuu Tunis jana usiku, baada ya kupigwa risasi kichwani.Lakini maafisa wa serikali wamesema, wao hawana taarifa yo yote kwa sasa.

Mwandishi: Mudhoon,Loay DW-Arabisch/Prema Martin
Mpitiaji:M.Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW