Je vijana wamehusishwa kikamilifu katika masuala ya uongozi?
10 Agosti 2018Jumuiya ya kimataifa itaadhimisha siku ya vijana tarehe 12 mwezi huu wa Agosti chini ya kauli mbiu ya nafasi salama kwa vijana. Fasili ya kaulimbiu hii ni kwamba wakati umewadia kwa vijana kuwezeshwa na kushirikishwa katika nafasi za uongozi ili kupata si tu jukwaa la kuwasilisha maoni yao, lakini pia kuhusishwa katika kutoa maamuzi kuhusu hali yao sasa na siku za usoni.
Kwa mujibu wa kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya vijana, dhana ya nafasi salama kwa vijana inaangazia uwezeshaji kwa vijana kupewa motisha ya kutimiza maslahi yao. Hii ina maana kuwa wakijenga uwezo wa kutoa maoni yao, kufanya maamuzi yanayohusu hali yao ya sasa na pia mustakabali wao katika mazingira ambapo hadhi yao inaheshimiwa, basi watajenga hisia chanya kushiriki katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Changamoto ya kutopewa nafasi na ukosefu wa nafasi ya ajira
Vijana nchini Uganda wakiwemo wakimbizi wanahisi kwamba hawajapewa nafasi na fursa muafaka za kutimiza ndoto zao. Ila wana mtazamo kuwa viongozi wa kisiasa huwatumia tu kwa ajili ya maslahi yao badala ya kuwahusisha moja kwa moja katika kubuni mikakati ya kuwa na jumuiya inayotambua kuwa vijana ndiyo nguvu na mhimili mkubwa wa nchi.
Vijana wana mtazamo kuwa changamoto kubwa kwao ni ukosefu wa nafasi za kazi hata baada ya idadi yao kubwa kukamilisha elimu ya juu. Aidha kuna hoja ya elimu wanayopokea vijana kutowawezesha kupata maarifa na stadi zinazohitajika na waajiri.
Changamoto kutokana na teknolojia
Kwa maoni ya baadhi ya vijana, teknolojia pia inazidi kuwa tishio kwao kwani waajiri wanapendelea kuwekeza katika mbinu na mitindo inayorahisisha kazi. Lakini kuna mtazamo kuwa vijana wajizatiti na kuwa wabunifu ili wasikose fursa za teknolojia kujenga mazingira ya ujasiriamali badala ya kusubiri kuajiriwa.
Vijana wakimbizi nao wanataka wasisahalike lakini kuwepo na mipango ya kuwahusisha katika mazungomzo ya kuleta amani katika nchi zao.
Huu ni mwaka wa 33 dunia ikiandimisha siku ya vijana.
Mwandishi: Lubega Emmanuel
Mhariri: Josephat Charo