1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je Wajerumani kupiga kura kujitowa Umoja Ulaya?

3 Julai 2016

Kufuatia Uingereza kupiga kura ya kujitowa Umoja wa Ulaya wananchi wengi wa Ulaya wanafikiri kwamba nchi zao pia zinapaswa kuitisha kura kama hiyo ya taifa lakini kwa Wajerumani vikwazo kufikia lengo hilo ni vikubwa mno.

Picha: ullstein bild - Teutopress

Kura ya maoni ya kihistoria ya Uingereza kujitowa katika Umoja wa Ulaya imepelekea kuongezeka kwa utashi wa kuwapa raia haki ya kuwa na usemi.Kabla ya kufanyika kwa kura hiyo ya kujitowa kwa Uingereza (Brexit) uchunguzi wa maoni umeonyesha takriban wazungu wa Ulaya 6,000 sawa na asilimia 45 ya waliohojiwa wamesema nchi zao zinapaswa kuwa na kura ya maoni kuhusiana na uwanachama wake kwa Umoja wa Ulaya.

Viongozi wa kisiasa wa sera kali za mrengo wa kulia nchini Ufaransa na Denmark wanatowa wito wa kuitishwa kwa kura ya maoni kuhusu uwanachama wa Umoja wa Ulaya katika nchi zao.Chama cha sera kali za mrengo wa kulia nchin Ujerumani kinachojulikana kama Chama Mbadala kwa Ujerumani (AfD) kinasema kitaitisha kura hiyo iwapo kitaingia bungeni katika uchaguzi mwa mwaka 2017.

Franz Wiese kutoka chama hicho amekaririwa akitamka kwamba "mwakani chama cha AfD kitaingia katika bunge la Ujerumani na suala la "Dexit" akimaanisha kujitowa kwa Ujerumani katika Umoja wa Ulaya litaongoza agenda yao.

Mwanzo mpya

Chama cha mrengo wa kushoto nchini humo pia kinadai kuwepo kwa "mwanzo mpya" katika Umoja wa Ulaya kwa mdahalo na kura kuhusu mustakbali wa Ulaya.Kiongozi wa chama hicho Sahra Wagenknecht hoja yake pia kuwa na kura ya maoni nchini Ujerumani juu ya kwamba sio kuhusu kujitowa bali juu ya baadhi ya mikataba na umoja huo.

Kiongozi wa chama cha mrengo wa kushoto Die Linke nchini Ujerumani Sahra Wagenknecht.Picha: Reuters/H. Hanschke

Wagenknecht ameliambia gazeti la Ujerumani la "Die Welt" kwamba chama chake bibi huyo kinataka kuubadili Umoja wa Ulaya ili kwamba usisambaratike na kuongeza kwamba wananchi wanapaswa kupatiwa fursa ya kupiga kura katika masuala muhimu kama vile makubaliano yanayopendekezwa ya biashara huru kati ya Ulaya na Marekani TTIP au mikataba mengine ya Ulaya.

Uingereza sio ya kwanza kuitisha kura ya maoni katika Umoja wa Ulaya: Hapo mwaka 1982 wananchi wa Greenland walipiga kura kujitowa katika kile wakati huo kilichokuwa kikijulikana kama Jumuiya ya Kuiuchumi ya Ulaya.

Kikwazo ni katiba

Hata hivyo katiba ya Ujerumani iliotungwa baada ya kipindi cha vita hairuhusu kulazimisha kura ya maoni ya taifa zima.

Aliyekuwa rais wa Ujerumani katika miaka 1950 Theodor Heuss.Picha: AP

Naye mwanasheria alieko Haidelberg Uwe Lipinski anasema Wajerumani wanaweza tu kupiga kura ya kujitowa Umoja wa Ulaya iwapo kwanza watabadili katiba kujumuisha kifungu cha kama vile "demokrasia ya moja kwa moja" katika ngazi ya taifa. Ni hapo tu ndio serikali ya Ujerumani au bunge itakapoweza kuitisha kura ya maoni.

Majimbo 16 ya Ujerumani yaliruhusiwa kuwa na mipango inayoanzishwa kwa juhudi za wananchi lakini kwa njia sio ya moja kwa moja kutokana na kuzingatia kipindi cha kale cha utawala wa Manazi nchini humo.

Katiba ya shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani inakubali tu kufanyika kwa kura ya maoni kwa kadhia mbili : kuhusiana na mabadiliko ya ardhi kiutawala au katika kesi za mageuzi ya katiba.Theodor Heuss mwanasiasa wa Ujerumani na rais kuanzia mwaka 1949 hadi mwaka 1959 ameita demokrasia ya moja kwa moja kuwa kishawishi kwa kila uhamasishaji unaozingatia hisia badala ya fikra.

Zaidi ya miongo saba baada ya kumalizika kwa vita vikuu vya kwanza vya dunia wakati umefika kufikiria juu ya mbadiliko ya katiba kujumuisha vitu kama vile "demokrasia ya moja kwa moja" Lipinski ameiambia DW na kutaja mifano ya Uswisi na mipango inayotokana na juhudi za wananchi katika ngazi ya majimbo nchini Ujerumani kuwa ni mifano mizuri ya kuigwa.

Wajerumani wengi wapinga kujitowa

Uchunguzi wa maoni nchini Ujerumani uliofanyika siku chache kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni ya Uingereza kuhusu uwanachama wake kwa Umoja wa Ulaya umeonyesha kwamba iwapo kungelikuwepo na kura ya maoni kama hiyo nchini Ujerumani matokeo yumkini yangelikuwa tafauti.

Bendera ya shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani.Picha: Colourbox

Asilimia 79 wangelipiga kura dhidi ya kujitowa Umoja wa Ulaya na ni asilimia 17 tu wangelipiga kura ya kujitowa mbapo asilimia 60 kati yao ni wafuasi wa chama cha AfD.

Miaka michache tu iliopita wakati wa kupamba moto kwa mzozo wa madeni barani Ulaya hapo mwaka 2012 Waziri wa Fedha Wolfgang Schäuble amesema Wajerumani wangelipanda kupiga kura ya maoni kuhusu katiba mpya tena ikiwezekana kwa haraka .

Amesema iwapo nchi itaendelea kuyaachilia makao makuu ya Umoja wa Ulaya yaiamulie masuala ya haki ya taifa kujiamulia mambo yake ametabiri hapo tena katiba ya Ujerumani itakuwa imefikia kikomo chake.

Mwanasheria Lipinski anaonya pengine hali inakaribia kufika huko kwani bunge la Ujerumani Bundestag limegeuka kuwa zana ya kutekeleza sheria ya Umoja wa Ulaya.

Mwandishi : Dagmar Breitenbach/Mohamed Dahman/

Mhariri :Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW