1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, Wamarekani wa asili ya Kiarabu watamuunga mkono Harris?

Sylvia Mwehozi
29 Julai 2024

Maafisa waandamizi kutoka vyama vyote vikubwa nchini Marekani wamekuwa wakitafuta uungwaji mkono kutoka kwa jamii ya Wamarekani wenye asili ya Kiarabu katika majimbo yenye umuhimu mkubwa katika uchaguzi wa Novemba.

Michigan 2024 | Kamala Harris
Makamu wa rais wa Marekani Kamala HarrisPicha: Kyle Mazza/NurPhoto/picture alliance

Harris ambaye yuko katika jitihada za kuteuliwa na chama chake cha Democratic, anaonekana kulikabili vyema jukumu la kuwashawishi wapiga kura wenye asili ya Kiarabu huko Michigan, jimbo ambalo Wademocrats wanaamini hapaswi kulipoteza katika uchaguzi wa Novemba. Viongozi wa kijamii wameelezea utayari wao wa kumsikiliza na baadhi tayari wamefanya mazungumzo ya awali na timu ya Harris.

"Mlango uko wazi tangu Biden alipojiuzulu" alisema Meya wa Dearborn Abdullah Hammoud. Viongozi wa Marekani wenye mizizi ya Kiarabu kama Hammoud wanatizama kwa ukaribu kama Harris atakuwa na sauti zaidi katika kutafuta usitishaji mapigano Mashariki ya Kati.  Wana shauku na ugombea wake lakini wanataka kuwa na uhakika kama atakuwa balozi mzuri wa amani na sio tu kuiunga mkono Israel. Lakini Harris atapaswa kuwa makini ili asiweze kujiweka kando na msimamo wa Biden katika vita vya Gaza, ambapo maafisa katika utawala wake wamekuwa wakifanya kazi kutafuta usitishaji mapigano nyuma ya pazia.

Imad Shehadeh, Mmarekani mwenye asili ya PalestinaPicha: DW

Mgawanyiko katika chama cha Harris ulishuhudiwa mjini Washington wiki iliyopita wakati wa ziara ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika bunge la Marekani. Baadhi ya Wademocrats waliunga mkono ziara hiyo, huku wengine wakipinga na kukataa kuhudhuria. Nje ya majengo ya bunge pia, kulifanyika maandamano ya kuiunga mkono Palestina.

Mwakilishi wa Michigan Rashida Tlaib ambaye ni mbunge pekee mwenye asili ya Palestina katika bunge la Marekani ambaye wilaya yake inajumuisha Dearborn, alibeba bango lenye ujumbe "mhalifu wa vita" wakati wa hotuba ya Biden. Harris hakuhudhuria kikao hicho.

Baadhi ya viongozi wenye asili ya kiarabu wanatafsiri hatua ya Harris ya kutohudhuria kikao hicho kama ishara ya kutia matumaini, ingawa wanatambua majukumu yake yanayoendelea kama makamu wa rais, ikiwemo mkutano wake na Netanyahu.

Mtihani wake wa kwanza ndani ya jamii hiyo, utaonekana wakati Harris atakapomchagua mgombea mwenza. Moja ya majina yanayotajwa ni gavana wa Pennsylvania Josh Shapiro ambaye amekuwa akikosoa hadharani waandamanaji wanaoiunga mkono  Palestina na yeye mwenyewe akiwa ni Myahudi.

Soma: Biden apongezwa kwa kujiondoa kwenye mbio za kuwania urais

"Josh Shapiro alikuwa mmojawapo ya watu waliokosoa maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu. Kwahiyo haitomtofautisha na Harris kama atamchagua kuwa mgombea wake mwenza. Hilo linaeleza kwa uwazi kwamba wataendeleza sera zilezile za Biden", alisema Rima Meroueh, mkurugenzi wa mtandao wa kitaifa wa jamii ya Wamarekani wenye asili ya Kiarabu.

Je Kamala anaweza kumshinda Trump katika uchaguzi 2024?

01:58

This browser does not support the video element.

Jamii hiyo ina matumaini kwamba kura zao zitakuwa na umuhimu katika majimbo yanayoamua kura za pande zote mbili ikiwemo Michigan. Jimbo hilo lina idadi kubwa ya Wamarekani wenye asili ya Kiarabu nchini Marekani na pia lilimuunga mkono kwa wingi Biden mwaka 2020. Mnamo mwezi Februari, zaidi ya wapiga kura 100,000 wa Democratic katika kura za mchujo za Michigan walipinga uungaji mkono usio na shaka wa utawala wa Biden kwa Israeli katika mashambulizi ya Oktoba 7 ya Hamas.

Soma pia: Hamasa kuhusu Kamala 'Kamala-mania' yafika Ulaya

Makundi yanayoongoza juhudi hizo yameitisha marufuku ya silaha dhidi ya Israel na usitishaji wa kudumu wa mapigano. Trump na kampeni zake, wakati huo huo pia wanatafuta kwa hali na mali uungaji mkono wa wapiga kura wa jamii hiyo ya Wamarekani wenye asili ya Kiarabu. Hata hivyo juhudi hizo zinatiwa doa na historia ya Trump na sera yake ya kuwachukia wahamiaji.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW