1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je watoto wa umri wa kati ya miaka 5-11 wanapaswa kuchanjwa?

29 Novemba 2021

Huku hali ya maambukizi ya virusi vya corona nchini Ujerumani ikizidi kuwa mbaya na mjadala kuhusu chanjo ukiendelea kupamba moto, swali jingine tete ni je watoto wadogo wanapaswa kuchanjwa? DW inaangazia suala hilo.

Israel | Covid-19 Impfung für Kinder
Picha: Oded Balilty/AP/dpa/picture alliance

Mnamo wiki iliyopita, shirika la kudhibiti dawa la Ulaya EMA liliridhia kwamba watoto walio na umri wa kati ya miaka 5-11 wanaweza kupewa chanjo ya BioNTech-Pfizer kwa jina Comirnaty. Shirika hilo lilisema viwango vya chanjo ya Comirnaty ni miligramu 10 pekee tofauti na miligramu 30 inayotolewa kwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 12. 

Hivi sasa kamati ya EMA kuhusu bidhaa za tiba kwa wanadamu inatathmini uwezekano wa kuidhinisha chanjo nyingine ya Moderna kwa jina Spikevax inayokusudiwa kutolewa kwa watoto wa umri ya kati ya miaka 6-11.

Lakini je watu wana maswali yapi kuhusu chanjo dhidi ya COVID kwa Watoto?

Kisa cha hivi karibuni cha mvulana mwenye umri wa miaka 12 aliyefariki muda mfupi baada ya kupewa dozi ya pili ya chanjo ya BioNTech katika mji wa Cuxhagen kaskazini mwa Ujerumani, kimechochea wasiwasi mwingi na dhana kadhaa kuhusu Watoto kupewa chanjo. Madai yanayotolewa ni kwamba mvulana huyo alifariki kwa sababu ya chanjo.

Soma: Guinea kuanza kuwachanja watoto dhidi ya COVID-19

Yapo madai ya kupotosha kuhusu chanjo za COVID-19 dhidi ya watoto. Lakini wataalamu wanasema watoto wenye miaka kati ya 5-11 wanaweza kupewa chanjo. Picha: Tom Brenner/REUTERS

Kulingana na maafisa wa afya wa Cuxhaven, madai hayo yanapotosha. Maafisa hao wametoa ufafanuzi baada ya uchunguzi kufanywa na ripoti kuwasilishwa kwa taasisi ya Ujerumani inayosimamia masuala ya chanjo (PEI). Ripoti ilisema mvulana huyo aliaga dunia kutokana na tatizo la moyo alilokuwa nalo awali. Na kwamba chanjo haiwezi kutajwa kuwa sababu pekee iliyochangia kifo chake.

Kwenye ripoti yake ya hivi karibuni kuhusu usalama, PEI ilitaja visa vitano kama hivyo ambavyo vimetokea tangu Septemba 30, vinavyoshukiwa kuhusiana na chanjo ya BioNTech-Pfizer kati ya watoto wenye umri wa kati ya miaka 12-17. Watoto watatu kati yao walikuwa na matatizo makali ya afya.

Soma: Hali ya COVID-19: Ujerumani iko mbioni kurejesha vizuizi

Profesa JörgDötsch wa chou kikuu cha Cologne kwa masuala ya tiba ya Watoto, ameliambia shirika la Habari DW kupitia barua pepe kwamba hakuna ushahidi wowote kwamba chanjo huweza kusababisho kifo kwa watoto. Ameongeza kwamba nchini Ujerumani, Watoto wanne wamefariki, lakini vifo hivyo havikuhusiana kwa vyoyote na chanjo walizopewa.

Je Watoto hawakabiliwi na hatari ya kuambukizwa?

La hasha. Katika ripoti yake ya hivi karibuni ya kila wiki, taasisi ya Marekani ya kudhibiti na kuzuia maradhi (CDC) ilieleza kwamba COVID-19 inaweza kusababisha madhara mabaya zaidi kwa watoto na hata wale ambao wamebaleghe.

Marekani yaidhinisha chanjo ya BioNTech/Pfizer kwa watoto wa 12-15

Chanjo ya BioNTech.Pfizer imeridhiwa na baadhi ya mamlaka kuwa salama kwa watoto.Picha: Tom Brenner/REUTERS

Maelezo ya kisayansi ya CDC yamefafanua kwamba watoto na waliovunja ungo wanaweza kuambukizwa COVID-19, kuwa wagonjwa na pia kueneza virusi.

Kwa mujibu wa takwimu kuanzia mwezi Machi mwaka huu, CDC ilibaini kwamba watoto walio na umri wa kati ya miaka 5-17, walikuwa na viwango vilivyokaribiana na watu wenye umri wa zaidi ya miaka 50 vya maambukizi na kuugua.

Wiki iliyopita CDC ilisema zaidi ya watoto 8,300 wa kati ya miaka 5-11 wamelazwa hospitalini kutokana na COVID-19 tangu mwezi Oktoba. Na kwamba takriban watoto 100 wamefariki. CDC ilitaja COVID-19 kuwa miongoni mwa visababishi kuu 10 vya vifo kwa watoto wenye umri uliotajwa.

Kulingana na Sean O'Leary, naibu mwenyekiti wa chuo cha madaktari wa wagonjwa (AAP) ambaye pia ni mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza kwa watoto katika chuo kikuu cha Colorado, zaidi ya watoto milioni 6.6 wameambukizwa virusi vya corona tangu janga hili lilipoanza. Kwenye maelezo yake kwa DW kwa njia ya barua pepe ameongeza pia kuwa watoto wameathirika kwa njia mbalimbali

Licha ya ushahidi kama huo, yapo madai yanayoenea kwamba uwezekano wa maambukizi ya virusi kwa watoto ni mdogo na unaoweza kupuuzwa hivyo hakuna haja ya watoto kupewa chanjo.

Mfano mwingine wa upotoshaji ni madai kwa njia ya video kwamba watoto 13 nchini Afrika Kusini walifariki mapema mwezi Novemba- baada ya kuchomwa chanjo ya COVID-19.

Madai hayo si kweli. Uchunguzi kwenye video hiyo  unathibitisha kuwa watoto walioonyeshwa waliuawa kwenye mkanyagano uliotokea Kenya mwaka 2020.

Mama Monica Strickland na bintiye mwenye umri wa miaka 11 na mvulana wa miaka 6 wakiashiria kuridhika baada ya watoto kupewa chanjo mjini San Diego, California Marekani Novemba 3, 2021.Picha: Mike Blake/REUTERS

Je chanjo inaweza kusababisha uvimbe wa moyo kwa watoto?

Madai mengine yanayoenea ni kwamba watoto wanaopewa chanjo ya COVID-19 wanaweza kupatwa na uvimbe wa mirija ya moyo na kuganda kwa damu.

Kulingana na O'Leary, kwa sasa hayo ni madai ya kupotosha. "chanjo za COVID zimefanyiwa uchunguzi na vipimo vingi na zinafany akazi vyema kwa asilimia 90. Madhara yao pia ni machache na madogo," amesema O'Leary.

Je Watoto wanapaswa kuchanjwa?

Wiki iliyopita, Israel ilianza mpango wa kutoa chanjo ya BioNTech-Pfizer kwa watoto wa kati ya miaka 5-11.

Hivyo kujiunga na orodha ndefu ya nchi ambazo zimeidhinisha chanjo kwa watoto wa umri huo.

Nchini Marekani, taasisi yake ya CDC iliridhia matumizi ya chanjo ya BioNTech-Pfizer baada ya kuidhinishwa na Mamlaka ya dawa na vyakula nchini humo (FDA).

Je watoto watakuwa katika hatari kubwa ya kufa wakichanjwa?

Kwa mujibu wa wataalamu, chanjo kwa watoto itawapa kinga na itawapa uhuru wa kushiriki shughuli muhimu kwa ukuaji wao ikiwemo kucheza na kutembeleana bila hofu.Picha: Mike Blake/REUTERS

Madai mengine ni kwamba watoto wako katika hatari ya kufariki baada ya kupata chanjo za COVID-19. Na kwamba hatari hiyo ni mara 50 kuliko virusi vyenyewe vya corona.

Madai hayo yalitolewa na Michael Yeadon, mwanasayansi wa zamani wa kampuni ya Pfizer ambaye amegeuka kuwa mwanaharakati na mpinzani mkubwa wa chanjo.

O’Leary amepuuza madai hayo akisema si kweli na hakuna ushahidi wowote unaoonesha kuwa kuna nafasi kubwa ya chanjo kusababisha kifo kuliko virusi.

Ripoti ya AAP imeeleza tangu janga kuanza hadi Novemba 18, watoto wasiopungua 636 walikuwa wamefariki dunia kulingana na takwimu zilizotolewa katika majimbo 45 ya Marekani.

Lakini hadi sasa hakujakuwa na kifo chochote cha mtoto ambacho kimesababishwa na chanjo ya covid-19.

Kwa kuhitimisha O’Leary amesisitiza kuwa ni muhimu kukinga afya ya watoto kwa kuwaruhusu kupata chanjo ili washiriki shughuli zao zote ambazo ni muhimu kwa ukuaji wa afya yao. Hatua hiyo itawapa nafasi pia kutembeleana na kucheza bila hofu.

Mwandishi: Mudge, Robert

Tafsiri: John Juma

Mhariri: Zainab Aziz