1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je zitarajiwe ahadi mpya kupambana na njaa duniani?

19 Novemba 2014

Wataalamu na wajumbe kutoka nchi 190 duniani wanashiriki mkutano wa kilele kuhusu njaa na lishe bora mjini Roma,Italia ikiwa ni baada ya miaka 22 tangu ulipofanyika mkutano wa ICN1

Mtoto akikomba sufuria,Gulu Uganda.Ni nembo ya shirika la FAO kuhusu njaa Afrika
Mtoto akikomba sufuria,Gulu Uganda.Ni nembo ya shirika la FAO kuhusu njaa AfrikaPicha: picture-alliance/dpa

Mjini Roma Italia unafanyika mkutano wa Kimataifa kuhusu njaa,na lishe bora duniani.Kwa mujibu wa ripoti kuhusu hali ilivyo asilimia 40 ya watu duniani hawana lishe bora,tatizo ambalo linabidi lipatiwe ufumbuzi.Hata hivyo suala linaloonekana kuzua mjadala ni kuhusu vipi na lini tatizo hilo litatuliwe.

Mkutano wa siku tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu suala la njaa na lishe bora unawakutanisha wataalamu,wajumbe wa mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka nchi 190 pamoja na kiongozi wa kanisa katoliki papa Fransis mjini Roma nchini Italia.Kiongozi huyo wa kidini aliyepangiwa kuhutubia mkutano huo kama bingwa wa kuwapigania watu masikini amekuwa akieleza hali hiyo kuwa ni ukosefu wa usawa duniani ambao ni kadhia kubwa.

Kilimo cha mahindi CameroonPicha: UN Photo / BZ

Shirika la Umoja wa Mataifa la kilimo na chakula duniani FAO limewahi kuandaa mkutano kama huo wa aina yake kwa mara ya kwanza kabisa kuhusu hali ya chakula duniani mwaka 1992 na kupiga hatua ndogo toka wakati huo. Kwa hivi sasa lakini inatajwa kwamba watu milioni 800 duniani wanakabiliwa na njaa kila siku huku wakipata lishe isiyokuwa bora kwa binadamu. Hata hivyo ikumbukwe kwamba idadi ya watu duniani imeongezeka tangu mwaka 1992 kutoka watu biliioni 5.5 hadi watu bilioni saba.Na kwahivyo kutokana na hesabu hizo inaamanisha kiwango cha watu wanaokabiliwa na njaa kinapungua

Shirika hilo la Fao linasema kwamba pamoja na idadi ya wenye njaa kupungua idadi ya wanaokosa lishe bora huenda ikaongezeka na kufikia watu milioni 1.2. Na kiasi kikubwa cha watu walioko katika kundi hilo la wanaokabiliwa na ukosefu wa lishe bora ni wanawake na watoto walioko chini ya umri wa miaka mitano wanasema wataalmu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa katika ripoti yao itakayowasilishwa mbele ya mkutano huo wa kilele utakaomalizika siku ya Ijumaa.

Mkutano kuhusu baa la njaa Afrika uliofanyika Roma,2011Picha: picture alliance/dpa

Aidha kwa mujibu wa mkurugenzi wa shirika hilo la FAO anayehusika na masuala ya lishe bora Anna Lartey pamekuweko na maendeleo kiasi katika kipindi cha miaka 22 iliyopita tangu ulipofanyika mkutano wa kwanza kuhusu chakula duniani na hasa maendeleo hayo yameonekana kwa China, ambako idadi ya wanaokosa lishe bora imepunguwa ingawa kiwango cha watu wanaokabiliwa na hali hiyo pamoja na watoto wanaokabiliwa na utapia mlo kimeongezeka katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara lakini pia katika nchi nyingine kama India,Pakistan au Indonesia ambako idadi ya walioko kwenye hali hiyo ni kubwa zaidi.

Mkutano wa wiki hii unatarajiwa kubainisha wazi kwamba kumalizwa kwa tatizo la ukosefu wa lishe bora kwa hali yoyote ile ni suala la msingi katika kuendeleza afya bora,maadili,siasa,ustawi wa jamii na hata uchumi.Halikadhalika mkutano huo unatarajiwa kuidhinisha mapendekezo 60 yaliyotolewa katika kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.

Mwandishi:Bernd Riegert/Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman