Jean Castex ndiye Waziri Mkuu mpya Ufaransa
3 Julai 2020Macron amemuagiza Castex kuunda serikali. Uteuzi wa Castex umetokea saa chache baada ya Edouard Philippe pamoja na serikali yake yote kutangaza kujiuzulu mapema Ijumaa.
Hatua hiyo inafuatia ahadi ya Macron kulifanyia mageuzi baraza lake la mawaziri baada ya uchaguzi wa manispaa Jumapili iliopita, ambao chama chake hakikufanya vizuri.
Kujiuzulu kwa Edouard Philippe kutafuatiwa na mabadiliko ya baraza la mawaziri yatakayompa Rais Macron fursa ya kuijenga upya timu atakayoingia nayo katika uchaguzi wa rais utakaofanyika mwaka 2022. Hata hivyo serikali iliyoko hivi sasa itaendesha shughuli za dharura hadi baraza jipya la mawaziri litakapoapishwa.
Kwenye mahojiano yaliyochapishwa leo Ijumaa na magazeti ya mjini Paris,Rais Macron ameelezea kwamba atamteua waziri mkuu mpya ambaye atachangia katika ujenzi na maridhiano ya Wafaransa.Philippe ambaye aliteuliwa kwenye wadhifa huo toka mwaka 2017, aliendesha baadhi ya mageuzi ambayo yalipingwa na wengi nchini mwake.
Ufaransa yapanga mageuzi magumu ya kiuchumi
Macron alipongeza kazi aliyoifanya Philippe na serikali yake kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita katika kile alichoelezea kuwa ni mazingira magumu. Mabadaliko hayo ya baraza la mawaziri yalitarajiwa baada ya duru ya pili ya uchaguzi wa manispaa Jumapili iliyopita, ambapo chama cha Kijani kilikishinda chama cha Macron katika miji mikubwa nchini humo.
Utafiti wa maoni ya raia unaonyesha kwamba asilimia 57 ya raia wa Ufaransa wamemuunga mkono Edaouard Philippe na kutaka aendelee kama waziri mkuu.
Rais Macron aliwatolea mwito raia wa Ufaransa kujiandaa katika mageuzi ya kiuchumu ambayo amesema kwamba yatakuwa magumu baada ya janga la virusi vya corona.
Macron ameliunga mkono pendekezo la Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen la euro bilioni 750 kama fungu la kuuokoa uchumi wa mataifa yaliyoathirika zaidi bila ya masharti ya kuzirejesha. Anasema walifanya kazi kwa pamoja na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel kwa ajili ya kuufikia mpango huo wa kufufua uchumi wa Ulaya.
Nchi za Ulaya ya Kusini zinaunga mkono mpango huo wa ufufuaji uchumi, ingawa kundi la nchi nne za Austria, Denmark, Uholanzi na Sweden zinapinga msaada mkubwa wa fedha bila ya masharti. Kwenye mahojiano yake na magezeti ya Ufaransa, Rais Macron amelionya kundi hilo la nchi nne akisema linapinga maslahi yake binafsi.