Jenerali Abdourahamane Tiane ajitangaza kiongozi mpya Niger
28 Julai 2023Jenerali Tiani ameomba kuungwa mkono katika uongozi wake, siku mbili baada ya wanajeshi kumpindua na kumshikilia Rais Mohamed Bazoum.
Uongozi huo mpya uliohusika na mapinduzi, katika taarifa yake iliyotolewa kwa njia ya televisheni umeyatahadharisha mataifa ya kigeni kutoiingilia kijeshi Niger. Taarifa hiyo imesema uingiliaji wowote kijeshi utakabiliwa na matokeo.
Wakati huo huo, Rais wa Kenya William Ruto amelaani mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika Niger akiita hatua hiyo kuwa ni kikwazo kikubwa kwa Afrika.
Amesema kuwa Jamhuri ya watu wa Kenya inaungana na dunia kulaani kwa nguvu zote kitendo kisicho cha kikatiba kinachochafua demokrasia kupitia mapinduzi ya kijeshi na inatoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa Rais Mohamed Bazoum anayeripotiwa kuwa amekamatwa na wajumbe wa kikosi cha ulinzi wa Rais.
Ufaransa yakataa kuutambua uongozi wa kijeshi wa Niger
Katika hatua nyingine, Ufaransa imesema haiwatambui viongozi waliotokana na mapinduzi ya kijeshi ya Niger na kwamba kiongozi halali pekee ni Rais Mohamed Bazoum.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Ufaransa imeisisitiza Jumuiya ya Kimataifa kutaka kurejeshwa kwa utaratibu wa kikatiba na serikali iliyowekwa madarakani na wananchi.
Kutokana na mapinduzi yaliyotokea Niger, Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS inatarajiwa kufanya mkutano Jumapili katika mji mkuu wa Nigeria Abuja. Awali Jumuiya hiyo ilitoa wito wa kuachiliwa kwa Rais Bazoum na kutaka katiba ifuatwe.
Soma zaidi: Umoja wa Ulaya wataka Bazoum aachiliwe huru
Niger, imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kiusalama tangu Bazoum alipochaguliwa kuwa Rais mwaka 2021 wakati makundi yenye itikadi kali yaliyokita mizizi yake nchini Mali yalipofanikiwa kudhidibiti baadhi ya maeneo, kuwauwa watu na kusababisha zaidi ya watu milioni 6 kuyahama makazi yao, kote katika ukanda wa Sahel.