1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jenerali Katumba wa Uganda anusurika shambulio la mauaji

Lubega Emmanuel 1 Juni 2021

Aliyekuwa mkuu wa majeshi nchini Uganda Jenerali Katumba Wamala amenusurika kuuawa na watu waliomiminia gari lake risasi asubuhi ya leo katika mtaa mmoja mjini Kampala

Uganda EU AMISOM Friedenstruppe General Katumba Wamala
Picha: DW/E. Lubega

Kulingana na walioshuhudia kisa hicho, watu wanne waliokuwa wakitumi pikipiki walilivamia gari la Jenerali Katumba Wamala na kulimiminia risasi katika mtaa wa Kisaasi mwendo wa saa tatu hivi asubuhi.

Baada ya watu hao ambao hadi sasa hawajatambulika kutoweka huku wakifyatua risasi hewani, imeelezwa kuwa jenerali huyo alitoka kwenye gari lake huku damu zikimchuruzika ubavuni na alikimbizwa hospitalini. Walioshuhudia kisa hicho wanasema.

Jenerali Katumba Wamala ambaye amekuwa waziri wa uchukuzi na ujenzi katika serikali ya Rais Yoweri Museveni ya muhula wa tano anatambulika kuwa mtu asiyependa makuu na hatembei na msafara wa walinzi kama wenzake walio kwenye ngazi za juu za serikali.

Kulingana na watu mbalimbali hii imetoa fursa kwa watu waliotaka kumuua kumvizia wakiwa na hakika kwamba hawezi kunusurika. Ila kwa bahati mbaya binti yake ambaye alikuwa akimsindikiza kwenda kuomboleza kifo cha mama mkwe wake pamoja na dereva wameuawa papo hapo. 

Mashuhuda katika eneo lilikofanyika shambulio dhidi ya KatumbaPicha: Lubega Emmanuel/DW

Mauaji ya aina hii ya watu mashuhuri yalikuwa yametulia kwa miaka miwili hivi tangu serikali ilipoweka kamera sehemu mbalimbali za miji na pia kuwahimiza watu binafsi kufanya hivyo kwenye makazi yao kuchangia katika kupambana na uhalifu huo. Lakini kulingana na maeneo alikovamiwa jenerali huyo jirani na nyumbani kwake, imebainikuwa kuwa hakuna vifaa hivyo. Ibrahim Juma ni mkazi wa Kisaasi.Museveni lazima aimarishe haki za binadamu

Polisi na wanajeshi wameanza uchunguzi wa jaribio hilo la kifo kwa jenerali Katumba Wamala ambaye anaaminiwa kuwa kiongozi mwaminifu sana kwa rais Museveni kutokana na nyadhifa mbalimbali ambazo ametumikia.

Kinachosubiriwa ni kuona kama wahusika katika mauaji hayo watakamatwa kwani tangu visa kama hivyo kutokea wakati aliyekuwa msemaji wa polisi Felix Kaweesi kuuawa pamoja na mbunge Ibrahim Abirga hakuna mtu aliyewahi kuhukumiwa kuhusiana na uhalifu huo.


 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW