1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jenerali Qassem Soleimani ni nani?

3 Januari 2020

Kwa raia wengi wa Iran ambao mashujaa wa taifa lao tangu mapinduzi ya kiislam wamekuwa ni maulamaa wenye sura zisizo na bashasha, Jenerali Qassem Soleimani alikuwa tofauti.

Iran Kommandeur Qassem Soleimani al-Quds Revolutionsgarden
Jenerali Qassem SoleimaniPicha: picture-alliance/abaca/Salampix

Kwa sehemu kubwa aliwakilisha taswira ya ustahamilivu wa kitaifa katikati ya miongo minne ya mbinyo wa Marekani. 

Jenerali Soleimani amekuwa shujaa nchini Iran kutokana na juhudi zake za kuipinga Marekani.

Kwa Marekani na Israel  Soleimani alikuwa kiongozi majununi, aliye nyuma ya vikosi vinavyoungwa mkono na Iran na anayehusika na wapiganaji wanaoitetea serikali ya rais Bashar Al Assad nchini Syria.

Kadhalika alibebeshwa wajibu wa vifo vya wanajeshi wengi wa Marekani nchini Iraq.

Soleimani alivishinda vishindo vya vita ya muda mrefu ya Iran dhidi Iraq miaka ya 1980 ili kuchukua nafasi ya kuongoza kikosi cha Quds kilicho sehemu ya kikosi kipana cha walinzi wa mapinduzi ya Iran.

Kikosi cha Quds ndiyo kinahusika na kampeni zote za kijeshi za Iran kwenye mataifa ya kigeni.

Aling´arishwa na uvamizi wa Marekani nchini Iraq

Picha: AFP/Iraqi Military

Jenerali huyo hakuwa akifahamika na wengi nchini Iran hadi mwaka 2003 wakati Marekani ilipoivamia kijeshi Iraq.

Wasifu na umashuhuri wake uliimarika hatua iliopelekea maafisa kadhaa wa Marekani kutoa wito wa kuuliwa kwake.

Muongo mmoja na nusu baadae Soleimani alifikia kuwa kamanda maarufu wa vita nchini Iran kiasi akipuuza miito ya umma kumtaka aingie kwenye siasa.

Kwa jenerali Soleimani nafasi ya kisiasa haikuwa na umuhimu mkubwa kwa sababu kutokana na ushawishi wake jeshini alifikia nafasi ya kuwa mtu mwenye nguvu nchini Iran pengine kuliko utawala wa kiraia.

Kifo chake kimekuja baada ya kuzushiwa mara kadhaa kufikwa na umauti.

Soleimani alizaliwa mwezi Machi mwaka 1957 na kukulia kwenye mji wa kihistoria wa Rabor nchini Iran.

Jina lake liianza kuzingatiwa alipopewa nafasi ya kuongoza kikosi cha Quds na kujenga usuhuba na kiongozi mkuu wa kidini Ayatollah Khamenei kiasi wakati mmoja ulamaa huyo alishiriki na kufungua dhifa ya harusi ya binti ya Jenerali Soleimani.

Jenerali aliyezongwa na lawama za Marekani?

Picha: AFP/Iranian Presidency

Akiwa mkuu wa kikosi cha Quds Soleimani alisimamia operesheni za kijeshi nje ya Iran na kuingia kweny euhasama na Marekani wakati wa vita vya Iraq akionekana kuwa mfadhili wa makundi ya wanamgambo wa kishia.

Marekani ilikilaumu kikosi cha Quds kwa shambulizi la Karbala lililowauwa wanajeshi wake watano pamoja na kutoa mafunzo na watengenezaji mabomu yayiotumika kuvilenga vikosi vyake.

Mwaka 2007 Marekani na Umoja wa Mataifa walimjumisha Soleimani katika orodha ya watu waliowekewa vikwazo lakini aliendelea kusafiri maeneo mbali mbali duniani.

Umashuhuri uliimarika zaidi wakati wa vita vya Syria na kutanuka kwa kundi linalojiita dola la kiislam. Iran ilimtuma Soleimani mara kadhaa nchini Syria kuongoza mashambulzii dhidi ya kundi la IS na makundi yanayopinga utawala wa Bashr Al Assad.

Jenerali huyo alipata mafanikio makubwa kwenye mapambano ya ardhini na alikuwa alama ya ushindi katika vita dhidi ya IS na kuendelea kulipa nuru jina lake, zaidi katika viwambaza vya dola na mioyoni mwa raia wengi wa Iran.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW