1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je,Opel iokolewe kwa fedha za walipoa kodi?

P.Martin - (DPA)23 Februari 2009

Mkutano wa viongozi wa Ulaya kutoka kundi la nchi tajiri zilioendelea na zinazoinukia kiuchumi G-20 kutafuta msimamo wa pamoja kuhusu mzozo wa uchumi na fedha duniani ni mada kuu lmagazetini Ujerumani leo Jumatatu.

Tunaanza na gazeti la NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG. Linasema:

Mkutano uliofanywa Berlin kujitayarisha kwa mkutano wa kilele ujao kuhusu mgogoro wa uchumi na fedha duniani,ulitoa ishara ya umoja.Hakuna hata mmoja aliepinga pendekezo la kuwa na sheria za kudhibiti masoko ya fedha. Pendekezo hilo limeungwa mkono hata na Uingereza ambayo tangu muda mrefu ilikuwa ikipinga kuingilia kati masoko ya fedha.

Likiendelea gazeti hilo linasema:

Muhimu zaidi ni kuchukuliwa hatua kali dhidi ya wale wanaohamisha pesa zao nchi za nje ili kujiepusha na malipo ya kodi.Lakini kuna suali,Je serikali mpya ya Marekani itakuwa na msimamo gani? Vile vile kuna mataifa mengine muhimu kama China na Urusi.Kwani juhudi zote za kuanzisha mfumo mpya wa fedha duniani,hazitoleta chochote bila ya kuungwa mkono na nchi hizo.Hatua ya kwanza imeshachukuliwa,lakini bado kuna mengi ya kutekelezwa.

Gazeti la REUTLINGER GENERAL ANZEIGER likiendelea na mada hiyo hiyo linasema:

Ni muhimu kuwa washirika wa Ulaya walio na usemi katika sekta ya uchumi hiyo jana waliweza kudhihirisha msimamo mmoja.Lakini katika siku hizi zijazo,tutaona jinsi yale yaliyokubaliwa yatakavyotekelezwa katika maisha ya kila siku.Mgogoro wa uchumi kwa mara nyingine tena,unatishia kuitenga Ulaya katika kambi ya Magharibi na Mashariki na upande mwingine Kaskazini na Kusini. Kweli,kuna haja ya kuwa na sheria mpya kudhibiti mifumo ya fedha duniani,lakini sheria tu hazitotosha kurejesha imani katika mifumo hiyo ya fedha.

Mgogoro wa kampuni ya magari Opel unaendelea kugonga vichwa vya habari magazetini wakati waajiriwa wakihofia kupoteza nafasi zao za ajira. Gazeti la NÜRNBERGER NACHRICHTEN linaeleza hivi:

Opel si kampuni ya kihivi hivi tu. Licha ya kumilikiwa na Marekani, kampuni hiyo kitamaduni ni ya Kijerumani.Serikali sasa inauliza iwapo kuna haja kweli ya kuinusuru au iiachie iende mrama.Ni sahihi kwa serikali kuweka masharti makali kabla ya kutoa fedha.Ukweli kwamba makampuni mfano wa Märklin au Schiesser yana majina mashuhuri,haimaanishi kuwa ndio lazima yaokolewe.Inapodhihirika kuwa bidhaa za makampuni hayo haziuziki basi viwanda vyake havina budi kufungwa.

Kwa upande mwingine gazeti la DARMSTÄDTER ECHO linaonya:

Mwaka huu wa chaguzi mbali mbali,wanasiasa wanataka kuonekana kama ni waokozi wa Opel.Lakini wapiga kura bora watazame kwa makini iwapo wao ndio watakaokuja kuubeba mzigo huo.Serikali inapaswa kujitahidi kwa kila njia kutafuta suluhisho pamoja na kampuni miliki General Motors ya Marekani na pia makampuni tanzu barani Ulaya.

Kwa kumalizia BRAUNSCHWEIGER ZEITUNG linauliza:

Je,serikali inaruhusiwa kutumia fedha za walipa kodi kuinusuru kampuni ya kitamaduni Opel ?Jawabu ni la.Si hilo tu,bali serikali haiwezi kuwa mdhamini wa mabilioni ya pesa au kufidia makosa yaliyofanywa na wamiliki. Kwani mambo yakienda kombo,fedha za walipa kodi hazitosaidia kunusuru nafasi za ajira-pesa hizo zitakwenda moja kwa moja katika kampuni miliki ya Kimarekani, General Motors.