1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM Ariel Sharon aepuka kashfa ya ufujaji fedha.

17 Februari 2005

Waziri mkuu wa Israel, Ariel Sharon, ameepuka kashfa ya ufujaji wa fedha za umma, lakini wizara ya sheria imeamua kumfikisha mahakamani mwanawe Sharon, Omri. Mwanachama huyo wa bunge la Knesset, mwenye umri wa miaka 40, anashtakiwa kwa kuelekeza fedha za misaada ya kigeni kudhamini kampeni za uchaguzi za babake za mwaka wa 1999. Shtaka rasmi dhidi ya Sharon lingeuhatarisha mpango wake wa kuyaondoa makazi ya wayahudi kutoka mkanda wa Gaza na sehemu za ukingo wa magharibi. Hapo awali bunge nchini Israel liliidhinisha mswada wa kuwalipa fidia wayahudi 8,000 wa mkanda wa Gaza ambao wataondolewa kutoka makazi yao baadaye mwaka huu. Wakazi hao wameendelea kufanya maandamano wakiupinga mpango huo wa kuwaondoa kutoka Gaza. Waziri mkuu Sharon, amesema Palestina itashirikishwa katika mpango huo ambao awali ulikuwa ufanywe na Israel pekee. Baraza lake la mawaziri litaupigia kura mpango huo Jumapili ijayo, huku kamati ya wakaazi wa kiyahudi, Yesha, ikiapa kuupinga pasipo kufanya vurugu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW