JERUSALEM : Blair kukutana na Abbas
10 Septemba 2006Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair anatazamiwa kukutana na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina katika ziara yake ya Mashariki ya Kati.
Mkutano wa waziri mkuu huyo na Abbas unakuja siku moja baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert. Olmert alisema yuko tayari kukutana na kiongozi huyo wa Palestina bila ya masharti yoyote yale.Hatua hiyo inafuatia wito wa Abbas wa kuwepo kwa mazungumzo mapya na Israel ya amani ya Mashariki ya Kati.
Blair amesema utulivu wa Mashariki ya Kati ni muhimu kwa dunia nzima na kuongeza kusema kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano huko Lebanon yaliodhaminiwa na Umoja wa Mataifa yanaweza kuupa msukumo mpya mchakato wa amani Mashariki ya Kati.
Hapo kesho Blair anaelekea Lebanon kwa mazungumzo na Waziri Mkuu Fuad Siniora.