Jerusalem. Israel yakubali kuachia fedha.
24 Desemba 2006Baraza la mawaziri la Israel limeamua kukabidhi dola milioni 100 zilizokuwa zimeshikiliwa ikiwa ni kodi za Wapalestina na kukabidhiwa kwa rais wa Palestina Mahmoud Abbas. Hii inafuatia mkutano mjini Jerusalem kati ya Abbas na waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert.
Israel ilitaka kupata uhakika kuwa fedha hizo hazitakabidhiwa kwa utawala wa Palestina wa chama cha Hamas.
Chama cha Hamas kilishinda uchaguzi mapema mwaka huu lakini kimekumbana na vikwazo kutoka mataifa ya magharibi kutokana na ukaidi wake wa kutotaka kukana matumizi ya nguvu dhidi ya Israel. Wadadisi wanasema kuwa mkutano kati ya Abbas na Olmerz ulikuwa na lengo la kuimarisha uwezo wa Abbas wakati anakabiliwa na hali ngumu ya kugombania madaraka na chama cha Hamas.
Olmert amesema kuwa mazungumzo zaidi na Abbas yanapangwa hapo baadaye.
Kamishna wa umoja wa Ulaya wa masuala ya kigeni Benita Ferrero-Waldner amesema kuwa mkutano huo unaleta matumaini ya kufufuliwa kwa juhudi za kuleta amani katika mashariki ya kati.