JERUSALEM: Makaburi ya watu mashuhuri yaharibiwa.
4 Aprili 2005Polisi wa Israel wameanza uchunguzi kufuatia uharibifu katika makaburi ya kihistoria likiwemo kaburi la kiongozi wa kiyahudi na aliyekuwa waziri mkuu wa Israel Yitzhak Rabin ambae aliuwawa kwa kupigwa risasi miaka kumi iliyopita.
Baadhi ya makaburi yaliyoharibiwa na kuchafuliwa kwa maandishi ya kashfa ni pamoja na kaburi la mkewe Yitzhak rabin marehemu bibi Leah na mzionisti Theodore Herzl na muanzilishi wa madhehebu ya Zioni nchini Israel marehemu Ben Gurion.
Habari zilizotangazwa kwenye televisheni ya Israel zimesema kuwa kamera za siri katika makaburi hayo zimenasa ukanda wa matukio katika makaburi ya mlima Herzl huko Jerusalem.
Wanasiasa wa mrengo wa kushoto katika bunge la Israel wamewalaumu wayahudi wanao pinga mpango wa waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon wa kuwahamisha masetla wa kiyahudi kutoka ukanda wa Gaza.
Marehemu Yitzhak Rabin aliuwawa kwa kupigwa risasi mwaka wa 1995 na mfuasi wa mrengo wa kulia uliopinga mpango wa amani baina ya Israel na Palestina.