JERUSALEM: Ndege ya Hezbollah yadenguliwa
8 Agosti 2006Ndege ya kundi la Hezbollah ambayo haikuwa na rubani imedenguliwa na ndege ya jeshi la Israel ilipoingia katika anga ya Israel.
Msemaji wa jeshi la Israel amesema ndege hiyo ilishambuliwa yapata kilomita 10 kutoka pwani ya Israel, kaskazini magharibi mwa mji wa Haifa.
Inasemekana ndege hiyo, iliyotengenezwa nchini Iran, ilikuwa njiani kuelekea eneo la kusini na haikuwa na silaha. Hata hivyo mabaki ya ndege hiyo yanafanyiwa uchunguzi.
Wakati huo huo, Israel imetangaza msako katika eneo la kusini mwa mto Litani. Walebanon wanaoishi katika eneo hilo hawataruhusiwa kutoka nje baada ya saa nne usiku na magari hayataruhusiwa kutembea barabarani isipokuwa magari yanayosafirisha misaada ya kiutu.
Msemaji wa jeshi la Israel amesema msako huo unalenga kuzuia silaha kupelekwa kwa wanamgambo wa Hezbollah kusini mwa Lebanon na haijulikani utaendelea kwa muda gani.
Wakati haya yakiarifiwa Israel imemrudisha nyumbani balozi wake nchini Venezuela kufuatia hatua ya rais wa nchi hiyo, Hugo Chavez, kuvipinga vita vya Israel dhidi ya kundi la Hezbollah.