JERUSALEM: Sharon akataa kufanya makubaliano mengine
11 Agosti 2005Waziri mkuu wa Israel, Ariel Sharon, hatafanya makubaliano mengine mbali na mpango wa kuyaondoa makazi ya wayahudi kutoka ukanda wa Gaza, unaotarajiwa kuanza wiki ijayo. Sharon amesema majengo ya Gaza yataendelea kubakia kuwa mali ya Israel na wala hatolijadili swala la Jerusalem. Pia amesema wakimbizi wa kipalestina wa mwaka wa 1948 hawataruhusiwa kurejea nchini Israel.
Matamshi yake katika runinga ya Israel, aliyatoa huku wapinzani wa mpango huo walipokuwa wakijitayarisha kufanya maandamano mjini Tel Aviv hii leo. Kundi la Yesha linasema wapinzani elfu 100 wataandamana.
Kiongozi wa Palestina, Mahmoud Abbas, amemushutumu Ariel Sharon kwa matamshi hayo na akasema hakuna aliye na haki ya kuyabadili makubaliano yaliyoafikiwa kati ya waisraeli na wapalestina. Abbas amesema hatoachilia ardhi yoyote ya Palestina kumilikiwa na Israel.