JERUSALEM. Sharon kukutana na Abbas
2 Juni 2005Waziri mkuu wa Israel, Ariel Sharon, ametangaza mpango wa kuandaa mkutano mwengine na rais wa Palestina, Mahmoud Abbas tarehe 21 mwezi huu. Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuziongezea nguvu harakati za kutafuta amani mashariki ya kati kabla kuanza mpango wa kuyaondoa makazi ya walowezi wa kiyahudi kutoka mkanda wa Gaza. Taarifa hiyo kutoka kwa ofisi ya Sharon imetolewa sambamba na mpango wa kuwaachilia huru wafungwa 400 wa kipalestina kutoka jela za Israel.
Rais wa Marekani George W. Bush amezihimiza pande hizo mbili kufufua tena mazungumzo ya amani. Sharon na Abbas walikutana mara ya mwisho huko Sharm el-Sheikh nchini Misri tarehe 8 mwezi Februari, ambako walikubaliana kusitisha mapigano ya miaka minne unusu. Makubaliano hayo yamechangia pakubwa kupunguza visa vya machafuko katika mkanda wa Gaza na ukingo wa magharibi.