1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JERUSALEM:Vifaru vya kijeshi vya Israel vimeingia Lebanon

22 Julai 2006

Vifaru vya Israel vimeingia ndani ya ardhi ya Lebanon huko kusini mwa nchi hiyo.Wanajeshi wa Israel pia wamefanya mashambulio kaskazini na eneo la kati la nchi hiyo na ambapo raia wanne na mwanamgambo mmoja wa Hezbollah wameuwawa na raia wengine saba wakajeruhiwa hii leo.

Mashambulio hayo pia yameharibu minara inayotumiwa kurushia matangazo ya televisheni na mawasiliano ya simu.Mashambulio hayo zaidi yalilenga minara ya vituo vya binafsi vya televisheni ikiwa ni pamoja na kituo cha Hezbollah al- manar,LBCI na vinginevyo.

Wanajeshi wa Israel wanaendelea kufanya mashambulio ya mabomu kusini mwa Lebanon na radio ya kijeshi ya Israel Al Mashriq imewaonya wakaazi wa vijiji 13 kusini mwa Lebanon kuondoka eneo hilo ifikiapo jioni hii.

Kiasi ya magari 10 ya kijeshi ya Israel yalivunja ua uliogawanya mpaka na kuingia upande wa Lebanon na kuzunguka kituo cha uangalizi cha umoja wa mataifa.

Israel imeongeza nguvu ya kikosi chake cha mpakani kwa kuwapeleka wanajeshi wa akiba zaidi ya 3000 katika eneo hilo.

Taarifa nyingine zinasema hivi punde wanamgambo wa Hezbollah wameishambulia ngome ya kijeshi ya Israel karibu na eneo la mpakani na kumjeruhi mwanajeshi mmoja wa Israel.

Hapo jana rais wa Lebanon Emile Lehud alitangaza kwamba jeshi lake liko tayari kupambana na wanajeshi wa Israel punde wakiivamia Lebanon.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW