Jeshi Burkina Faso lakemewa licha ya uungwaji mkono
26 Januari 2022Wafuasi wa utawala mpya wa kijeshi nchini Burkina Faso wameandamana jana katika mitaa ya mji mkuu Ouagadougou wakati Umoja wa Mataifa, Ufaransa na nchi jirani za ukanda wa Sahel zikilaani mapinduzi hayo ya karibuni ya kijeshi.
Soma pia: Burkina Faso kukabiliwa na hali tete zaidi?
Maafisa wa jeshi walimkamata Rais Roch Marc Christian Kabore Jumatatu wakati kukiwa na hasira kuhusu anavyoushughulikia uasi wa itikadi kali.
Koloni hilo la zamani la Ufaransa sas aliko mikononi mwa chama cha Patriotic Movement for Preservation and Restoration – MPSR, jina la utawala wa kijeshi ukiongozwa na Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba. Mamia kadhaa ya watu walikusanyika katikati mwa mji mkuu Ouagadogou wakisherehekea na kupeperusha bendera kuonyesha uungaji mkono kwa wanajeshi wa mapinduzi. Huyu hapa mmoja wao "Vikwazo vya ECOWAS nchini Mali havitutishi. Kwa sababu tuko Burkina Faso, sisi ni waBurkinabe na tuna heshima yetu. Burkina Faso na Mali zinafanana. Kwa hiyo tunapinga vikwazo. Jeshi lilichukua madaraka ili kurekebisha mambo Burkina Faso. Hicho ndio tunachojali. ECOWAS, bakini huko huko."
Jeshi lilitangaza jana kurejea kwa safari za angani wakati likifungua mipaka ya ardhini kwa magari yanayosafirisha bidhaa za kiutu, kijeshi na bidhaa muhimu.
Afrika Magharibi imekumbwa na matukio matatu ya mapinduzi katika muda wa chini ya miezi 18, kuanzia Mali Agosti 2020, kisha Guinea Septemba 2021. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekashifu mapinduzi hayo ya mara kwa mara akisema hayakubaliki, akiongeza kuwa jamii za kidemokrasia ni thamani ambayo lazima ihifadhiwe. "Nina wasiwasi mkubwa kuhusu mapinduzi ya karibuni Burkina Faso. Jukumu la jeshi ni kulinda nchi zao na watu wao, na sio kuzishambulia srikali na kupigania madaraka." Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi – ECOWAS, ambayo inajumuisha Burkina Faso, iliandaa mkutano maalum wa kilele na kutoa taarifa iliyolaani vikali mapinduzi hayo. Uingereza na Afrika Kusini pia ilijiunga na sauti za ukosoaji.
Muungano wa kijeshi wa nchi za Sahel unaopigana hidi ya uasi wa itikadi kali – G5 Sahel ambao unajumuisha Chad, Mali, Mauritania na Niger, ulikemea kile ulichokiita jaribio la kuvuruga utaratibu wa kisheria nchini Burkina Faso ambayo ni mwanachama wake watano.
Soma pia: Burkina Faso: Milio mikubwa ya bunduki yarindima kwenye kambi kadhaa za jeshi
Haijulikani mahali waliko Kabore, Waziri Mkuu Lassina Zerbo na maafisa wengine waandamizi. Jeshi lilisema operesheni za kumuondoa Kabore zilifanyika bila umwagaji damu na bila ya ukatili wowote wa kimwili dhidi ya watu waliokamatwa na ambao wanashikiliwa katika eneo salama na kwa heshima ya hadhi yao.
Kabore alichaguliwa mwaka wa 2015, akijinadi kama nguzo ya matumaini baada ya utawala wa muda mrefu wa Blaise Compaore aliyeongoza kwa mkono wa chuma, na ambaye aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya 1987.
afp,dpa,ap,reuters