1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi Gabon lampindua rais Ali Bongo Ondimba

30 Agosti 2023

Viongozi wa kijeshi nchini Gabon wametangaza kuchukuwa madaraka, siku chache baada ya taifa hilo la Afrika ya Kati kufanya uchaguzi uliomrejesha madarakani rais Ali Bongo Ondimba kwa muhula wa tatu.

Gabuns Präsident Ali Bongo Ondimba
Picha: Witt Jacques/Pool/ABACA/picture alliance

Kundi la maafisa wa jeshi nchini Gabon lililojiita Kamati ya Mpito na Urejeshaji wa Taasisi, CTRI, limetangaza kusimamisha taasisi zote na kufunga mpaka mara moja, kufuta matokeo ya uchaguzi. Milio ya risasi ilisikika katika mji mjuu Libraville.

CTRI imeamua "kuwekwa mwisho kwa utawala wa sasa," alisema moja ya maafisa hao. Tangazo hilo limekuja saa chache baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza Bongo kuwa mshindi wa uchaguzi kwa kupata asilimia 64.27 ya kuta. Mpinzani mkuu wa Bongo, Albert Ondo Ossa, alipata asilimia 30.77 ya kura, ilisema tume hiyo.

Huu ndiyo ungekuwa mhula wa tatu wa Bongo. Familia yake imetawala kwa zaidi ya miaka 55, baada ya kutwaa madaraka mwaka 2009 kutoka kwa baba yake Omar Bongo, alietawala kuanzia 1967 hadi kifo chacke. Gabon ina watu karibu milioni 2.3, wengi wao wakiishi kwenye umaskini.

Soma pia: Gabon inafanya uchaguzi wa Rais wabunge na serikali za mitaa

Uchaguzi wa Agosti 26 ulisababisha ukosoaji baada ya serikali kuzuwia upatikanaji wa huduma za intaneti huku kura zikiendelea kuhesabiwa mwishoni mwa wiki. Zaidi ya hapo, amri ya kutoka nje ilitangazwa kuanzia saa moja jioni hadi 12 asubuhi na vituo kadhaa vya Redio France vilipigwa marufuku kutangaza.

Wanajeshi wa Gabon wakitangaza hatua ya kuipindua serikali kupitia kituo cha televisheni ya taifa cha Gabon 24.Picha: Gabon 24/AFP

Uchaguzi huo ulikumbwa na ukosefu wa waangalizi wa kimataifa na maombi ya waandishi habari wa kigeni kupewa vibali vya kuripoti yalikataliwa. Mapinduzi hayo yamekuja chini ya mwezi mmoja baada ya walinzi wa Rais wa Niger kumpindua rais aliechaguliwa kidemokrasia Mohamed Bazoum. Viongozi wa kijeshi pia walichukuwa madaraka nchini Mali na Burkina Faso, na kusababisha wasiwasi kuhusu demokrasia katika kanda hiyo.

Tasisi zote zimevunjwa

"Katika jina la watu wa Gabon...tumeamua kulinda amani kwa kuhitimisha utawala wa sasa," walisema maafisa hao. Tangazo hilo lilitolewa kupitia kituo cha Televisheni cha Gabon 24 kwa niaba ya kundi la CTRI.

Likidai kuwakilisha vikosi voyte vya usalama vya Gabon, maafisa hao walitangaza kuvunjwa kwa "taasisi zote za jamhuri."

Soma pia: Uchaguzi wa rais Gabon: Bongo kuchuana na wagombea 18

Waliangazia "utawala usio wa uwajibikaji, utawala usiotabirika" na kusababisha kudorora kwa mazingira ya kijamii, kama sababu za uingiliaji wao, unaokusudia kurejesha amani kwa kuhitimisha utawala wa sasa.

Wasiwasi mkubwa tangu uchaguzi

Mzozo umeongezeka kufuatia uchaguzi wa Jumamosi, ambako Bongo alilenga kuendeleza utawala wa miaka 55 wa familia yake katikati mwa miito ya mabadiliko kutoka kwa upinzani katika taifa hilo lenye utajiri wa rasilimali lakini maskini.

Mgombea wa upinzani katika uchaguzi wa Gabon Albert Ondo Ossa alishika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 30 ya kura.Picha: Steeve JORDAN/AFP

Wasiwasi kuhusu uwazi uliongezeka kutokana na kutokuwepo kwa waangalizi wa kimataifa, kusitishwa kwa matangazo ya vituo vya kigeni, na ukataji wa nchi nzima wa mtandao wa intaneti pamja na amri ya kutotoka nje. Hakukuwa na tamko mara moja kutoka serikalini.

Jaribio hilo la mapinduzi limetokea karibu mwezi mmoja baada ya wanajeshi waasi nchini Niger kuipindua serikali iliyochaguliwa.

Mnamo mwaka 2019, wanajeshi walikuwa wametangaza kupitia redio ya taifa kwamba walikuwa "wameunda baraza la taifa la urejeshaji" kumuondoa rais Ali Bongo.

Soma pia: Rais wa Gabon Ali Bongo kugombea tena urais

Jaribio hilo la mapinduzi lilidumu kwa chini ya wiki moja baada ya vikosi vya jeshi kuvamia kituo hicho na wapangaji nane wa njama hiyo kukamatwa na wawili kuuawa.

Wakati huo huo, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrel, amesema mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya watajadili hali nchini Gabon. Mapinduzi nchini Gabon yatasababisha ukosefu zaidi wa utulivu katika kanda, alisema Borrel.

Chanzo: Mashirika

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW