1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Jeshi la Iran laapa kulinda mali za umma kufuatia ghasia

Saleh Mwanamilongo
10 Januari 2026

Jeshi la Iran lasema litalinda miundombinu na mali ya umma, likiwataka Wairani kuzuia njama za adui huku mamlaka zikikandamiza maandamano.

Iran | Gwaride la kijeshi mjini Tehran
Jaji Mkuu wa Iran Gholamhossein Mohseni-Ejei, amesema adhabu kwa waandamanaji itakuwa nzito na ya haraka isiyokuwa na hurumaPicha: Vahid Salemi/AP Photot/picture alliance

Taarifa ya jeshi la Iran ilitolewa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutoa onyo jipya kwa viongozi wa Iran siku ya Ijumaa, na baada ya Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio kutangaza siku ya Jumamosi kwamba "Marekani inawaunga mkono watu jasiri wa Iran."

Machafuko yaliendelea usiku kucha. Vyombo vya habari vya serikali vilisema kuwa jengo la manispaa lilichomwa moto mjini Karaj, magharibi mwa Tehran, na kuwalaumu "wachochezi kwa ghasia". Televisheni ya taifa ilirusha picha za mazishi ya wanachama wa vikosi vya usalama ambao ilisema waliuawa wakati wa maandamano katika miji ya Shiraz, Qom na Hamedan.

"Makundi ya kigaidi" yanajaribu kudhoofisha usalama

Khamenei akosoa maandamano dhidi ya serikali, IranPicha: Office of the Iranian Supreme Leader/WANA/REUTERS

Mamlaka inaendelea kuweka zuio la mtandao wa intaneti. Shahidi mmoja magharibi mwa Iran, aliyepatikana kwa simu, alisema Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) walikuwa wametumwa katika eneo hilo na walikuwa wakifyatua risasi, akakataa kutajwa jina kwa sababu za usalama.

Jeshi la Iran linafanya kazi kivyake na IRGC — kikosi maalumu kilichopewa jukumu la kulinda Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran — ambacho mamlaka imekuwa ikikituma kukandamiza machafuko ya awali. Vikosi vyote viwili vinaongozwa na Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei.

Katika taarifa iliyochapishwa na tovuti za habari zisizo rasmi kikamilifu, jeshi liliilaumu Israel na "makundi ya kigaidi yenye uhasama" kwa kujaribu "kudhoofisha usalama wa umma wa nchi".

"Jeshi, chini ya uongozi wa Amiri Jeshi Mkuu, pamoja na vikosi vingine vya usalama, mbali na kufuatilia mienendo ya adui katika eneo hilo, litalinda kwa uthabiti maslahi ya taifa, miundombinu ya kimkakati ya nchi, na mali ya umma", taarifa hiyo ilisema.

Maandamano mapya yazuka Iran licha ya kufungwa kwa intanetiPicha: UGC/DW

Maandamano yameenea katika sehemu kubwa ya Iran katika wiki mbili zilizopita, yakianza kama majibu ya kupanda kwa kasi kwa mfumuko wa bei, lakini yakageuka haraka kuwa ya kisiasa huku waandamanaji wakitaka watawala wa kidini waondoke madarakani. Mamlaka zimezituhumu Marekani na Israel kwa kuchochea "ghasia".

Shirika la haki za binadamu la Iran, HRANA, lilisema lilikuwa limerekodi vifo 65 hadi Januari 9, vikiwemo vifo vya waandamanaji 50 na wanachama 15 wa vikosi vya usalama. Shirika la haki za binadamu lenye makao yake Norway, Hengaw, lilisema zaidi ya watu 2,500 walikuwa wamekamatwa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Katika nchi yenye historia ya upinzani uliogawanyika dhidi ya utawala wa kidini, Reza Pahlavi mwanaye kiongozi wa zamani wa Iran aliyepinduliwa katika Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 ameibuka kama sauti muhimu iliyo nje ya nchi, akihamasisha maandamano hayo.

Lengo la waandamani ni kudhibiti maeneno ya miji

Picha: Iran state TV/AP Photo/dpa/picture alliance

Katika wito wake wa hivi karibuni kupitia jukwaa la mtandao ya kijamii wa X, Reza Pahlavi anayeishi Marekani alisema:

"Lengo letu si tena kutoka tu mitaani, lengo ni kujiandaa kutwaa vituo vya miji na kuvidhibiti."

Pia aliwataka "wafanyakazi na waajiriwa katika sekta muhimu za uchumi, hasa usafirishaji, pamoja na mafuta, gesi na nishati," kuanza mgomo wa kitaifa.

Trump alisema Alhamisi kuwa hakuwa na mwelekeo wa kukutana na Pahlavi, ishara kwamba alikuwa akisubiri kuona hali ya mgogoro itakavyokwenda kabla ya kumuunga mkono kiongozi wa upinzani. Trump, ambaye aliishambulia Iran kwa mabomu msimu wa joto uliyopita na kuionya Tehran wiki iliyopita kuwa Marekani ingeweza kuwasaidia waandamanaji, alitoa onyo jingine Ijumaa akisema:

"Ni afadhali msianze kupiga risasi, kwa sababu nasi tutaanza kupiga risasi". Aliongeza: "Natumaini tu waandamanaji wa Iran watakuwa salama, kwa sababu kwa sasa ni mahali hatari sana."

Ijumaa, Khamenei aliwatuhumu waandamanaji kwa kutenda kwa niaba ya Trump, akisema wachochezi walikuwa wakishambulia mali ya umma na akaonya kuwa Tehran haitavumilia watu wanaotenda kama "mamluki wa wageni".

Miito ya kimataifa kwa viongozi wa Iran

Umoja wa Ulaya umekasirishwa na hatua hiyo na kutoa wito kwa utawala nchini humo kurejesha huduma hiyo mara moja na kukosoa vurugu za aina yoyote dhidi ya waandamanajiPicha: UGC

Viongozi wa Ufaransa, Uingereza na Ujerumani walitoa tamko la pamoja Ijumaa kulaani mauaji ya waandamanaji na kuyataka mamlaka ya Iran kujizuia kutumia vurugu. Mamlaka yameeleza maandamano kuhusu uchumi kuwa halali, huku yakilaani kile wanachokiita wachochezi wa vurugu na kukabiliana nao kwa kutumia vikosi vya usalama.

Uongozi wa kidini wa Iran umewahi kupitia mawimbi kadhaa ya machafuko hapo awali, yakiwemo maandamano ya wanafunzi mwaka 1999, yale ya kupinga matokeo ya uchaguzi mwaka 2009, maandamano dhidi ya matatizo ya kiuchumi mwaka 2019, na maandamano ya "Mwanamke na Uhuru" ya mwaka 2022.

Chanzo : Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW