1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Kongo lawasaka waasi wa FDLR mkoani Kivu Kaskazini

Saleh Mwanamilongo
27 Septemba 2024

Msako huo unayalenga pia makundi mengine ya wapiganaji ambayo yalikuwa yakiliunga mkono jeshi hilo dhidi ya waasi wa M23 kwenye mkoa wa Kivu ya Kaskazini.

Mashariki mwa Kongo yenye utajiri mkubwa wa madini imekuwa ikikumbwa na ghasia za ndani na za mipakani kwa miongo mitatu iliyopita
Mashariki mwa Kongo yenye utajiri mkubwa wa madini imekuwa ikikumbwa na ghasia za ndani na za mipakani kwa miongo mitatu iliyopitaPicha: Djaffar Sabiti/REUTERS

Hali imerudi kuwa tulivu Ijumaa kwenye mtaa wa Nyiragongo karibu na mji wa Goma, baada ya mapigano makali kushuhudiwa jana alhamisi kwenye mji wa Rusayo. Duru zinasema kuwa jeshi la Kongo liliendesha operesheni za kijeshi dhidi ya waasi wa Rwanda wa FDLR na wapiganaji wa kundi la APCLS.

Mambo kawaya, mwenye kiti wa asasi za kiraia kwenye mtaa huo wa Nyiragongo amesema mamia ya wakaazi wa eneo hilo wamelazimika kukimbia.

"Kwa kweli mapigano yamezuka toka juzi na jana (alhamisi), na kwa kweli yalikuwa mapigano makali kwa sababu zilaha nzito zilisikia pamoja na mabomu. Jeshi la taifa (FARDC) liliendesha mapigano dhidi ya makundi yawapiganaji wanaloliunga mkono.", alisema Kawaya.

Duru za hospitali na mashirika ya kibinadamu yamesema raia watatu waliuawa na wengine 21 kujeruhiwa wakati wa mapigano karibu na kambi ya wakimbizi ya Lushagala, karibu na mji wa Goma. Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP ni kwamba maafisa watatu wa kundi la wapiganaji wa APCLS pia waliuliwa kufuatia mapigano hayo. Kundi hilo ni miongoni mwa makundi yanayoliunga mkono jeshi la Kongo kupambana na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda.

''Ni Wakongo wanaolengwa zaidi''

Maelfu ya wakaazi wa mitaa za kusini mwa mkoa wa Kivu ya Kaskazini wanaendelea kuhayama makazi yao kufuatia machafukoPicha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Kwa mujibu wa duru za kiusalama ni kwamba msako huo wa jeshi la Kongo unafuatia makubalano baina ya Rwanda na Kongo yaliofikiwa mwezi Julai chini ya upatanishi wa Angola, ili kumaliza machafuko huko KIvu. Moja ya masharti ya Rwanda kwa Kongo ilikuwa ni kulitokomeza kundi la waasi wa FDLR huko Kivu ya Kaskazini. Hata hivyo jeshi na maafisa wa serikali ya Kongo hawakuelezea sababu za operesheni hizo.

Mambo Kawaya amesema mapigano hayo baina ya jeshi la Kongo dhidi ya washirika wake yameibua msangao na wasiwasi mkubwa.

"Hatujafahamu wazi kipi kinaendelea kufanyika. Upande wa serikali umesema wamezilenga ngome za waasi wa Rwanda wa FDLR, lakini ukiangalia kwa karibu kinachofanywa ni Wakongo wanaolengwa zaidi.", alisema Mambo Kawaya mkuu wa asasi za kiraia huko Nyiragongo.

Makundi kadhaa yenye silaha na yanayoiunga mkono serikali ya Kongo, yanayojulikana kwa jina maarufu "Wazalendo" yamepiga kambi kwenye viunga vya mji wa Goma, katika kile wanachoelezea kuwa ni kuepusha mji huo kutekwa na waasi wa M23.