1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi kuzuia ghasia Venezuela

18 Mei 2017

Serikali ya Venezuela imesema itapeleka vikosi katika ukanda unaokabiliwa na machafuko yaliyotokea wakati wa maandamano ya kuipinga serikali, huku Marekani ikitaka Umoja wa Mataifa kuuzuia mzozo huo

Venezuela Anti-Regierungs Proteste
Picha: Reuters/C.G. Rawlins

Kifo cha kijana wa kiume wa umri wa miaka 15 kilisababisha maandamano yaliyodumu wiki kadhaa nchini Venezuela na kusababisha vifo vya kiasi ya watu 43, idadi ambayo inalinganishwa na ile iliyotokea wakati wa machafuko yaliyotokea mnamo mwaka 2014.

Uporaji na mashambulizi dhidi ya majengo ya idara za usalama vilianza ghafla majira ya usiku katika jimbo la Tachira, lililoko mpakani mwa Colombia, zimesema mamlaka. Idara ya mwendesha mashitaka ya nchi hiyo, imesema kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba kijana huyo aliuwawa kwenye maandamano.

Waziri wa ulinzi wa Venezuela Vladimir Padrino amenukuliwa kupitia kituo cha televisheni cha taifa VTV akisema ameagiza kupelekwa kwa walinzi 2,000 na vikosi maalumu 600 huko Tachira.  

Marekani inashinikiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzuia mzozo huoPicha: picture alliance/dpa/L. R. Lima

Marekani kupitia balozi wake katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley imeonya kwamba mzozo wa Venezuela unaendelea kuwa mbaya zaidi na unaweza kusambaa na kufikia vita vya wenyewe kwa wenyewe kama vile vinavyoendelea nchini Syria.

Balozi wa Venezuela katika Umoja wa Mataifa, Rafael Ramirez kwa upande wake amekataa mpango wa Marekani unaoshinikiza uingiliaji wake kwenye mzozo huo na kuwaambia wanahabari kwamba mzozo huo ni wa ndani.

Mabalozi kutoka nchi za Bolivia na Uruguay ambao ni wanachama wa baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa, wakati Venezuela si mwanachama kwa pamoja wamesema mzozo wa Venezuela unatakiwa kumalizwa na wao wenyewe,, na si katika ngazi ya kimataifa.

Bolivia na Uruguay jana Jumatano ziliungana na Venezuela, katika kupinga vikali jaribio la Marekani kutaka kuuzungumzia mzozo wa kiuchumi na kisiasa unaoendelea nchini Venezuela mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mzozo huo ulioasambaa nchi nzima ulianzia kwa waandamanaji waliokuwa na ghadhabu dhidi ya rais Maduro na namna anavyokabiliana na majanga ya kisiasa na uchumi nchini humo. watu 43 wamekufa tangu Aprili 1, amesema mwendesha mashitaka.

Mzozo huo pia umeibua wasiwasi kwa jamii ya kimataifa. Wapinzani wanataka kufanyika kwa uchaguzi na kuachiwa kwa wafungwa wa kisiasa, pamoja na kukubaliwa kwa misaada ya kibanaadamu wakati ambapo kuna upugnufu mkubwa wa chakula na dawa nchini humo. 

Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE/AFPE.
Mhariri: Yusuf Saumu