Jeshi la anga la Libya lazidi kurudi nyuma
24 Machi 2011Mashambulizi yanawalazimisha wanajeshi watiifu kwa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi kurudi nyuma, ingawa bado wanashambulia kambi za waasi katika miji ya Misrata ulioko magharibi na Adjabiya ulioko mashariki.
Kituo cha televisheni cha Al-Jazeera kimetangaza kuwa kikosi hicho cha muungano wa kimataifa kinaendelea na mashambulizi yake dhidi ya vikosi vya Kanali Gaddafi kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Wakati huo huo, Uingereza imetangaza kuandaa mkutano wa kimataifa utakaojadili maendeleo ya kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Libya. Mkutano huo utakaofanyika Jumanne ijayo mjini London, utalenga zaidi kuhusu maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na mahitaji ya kibinaadamu ya watu wa Libya.
Bado haijafahamika jukumu ambalo Jumuiya ya Kujihami ya NATO italitimiza katika kutekeleza operesheni ya kuzuia ndege kuruka kwenye anga ya Libya, ambayo kwa sasa inaongozwa na Marekani. Rais Barack Obama wa Marekani anataka kukabidhi jukumu hilo haraka iwezekanavyo. Wiki iliyopita, Ujerumani haikupiga kura katika baraza hilo la usalama.
Aidha, juzi Jumanne Ujerumani ilijiondoa katika operesheni za NATO kwenye Bahari ya Meditteranean kutokana na jumuiya hiyo kujiingiza katika mzozo wa Libya na kurejesha udhibiti wa meli nne za kijeshi chini yake. Lakini katika hatua ya kukisaidia kikosi cha muungano nchini Libya, baraza la mawaziri la Ujerumani jana lilipitisha mipango ya kupeleka wanajeshi wa kurusha ndege za uchunguzi za NATO nchini Afghanistan.