1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yadaiwa kutekeleza mauaji Ukingo wa Magharibi

11 Aprili 2022

Wizara ya afya ya Palestina imeripoti kwamba wanajeshi wa Israel wamemuua kwa kumpiga risasi mwanamme mmoja wa Kipalestina karibu na mji wa Bethlehem katika eneo lililozingirwa la Ukingo wa Magharibi

West Bank | Israel - Palästinenser Konflikt | israelische Truppen im Nur Shams Flüchlingslager
Picha: Israeli Army/Handout/AA/picture alliance

Jeshi la Israel limesema limemshambulia kwa risasi mtu aliyerusha mabomu kwenye gari la Israel lililokuwa katika barabara kuu ya Ukingo wa Magharibi jana Jumapili jioni. Kisa hicho kimeongeza idadi ya Wapalestina waliouwawa na wanajeshi wa Israel kufikia wanne ndani ya saa 24, miongoni mwao akiwa mwanamke aliyekuwa hana silaha aliyepigwa risasi na kuuwawa karibu na kituo cha ukaguzi cha Bethlehem.

Maafisa wa wizara ya afya ya Palestina wamemtambua mwanamume huyo aliyeuwawa hapo jana kama Muhammed Ali Ahmed Ghoneim aliye na miaka 21. Kijana mwengine wa miaka 17 , Mohammed Zakarna pia ameripotiwa kufariki leo Jumatatu baada ya kujeruhiwa kwa risasi zilizorushwa kutoka upande wa Israel katika mji wa Jenin ulioko pia katika Ukingo wa Magharibi siku ya Jumamosi.

Tangu hapo jana wanajeshi wa Israel wameendelea kushika doria mjini Jenin ambao ni ngome ya wanamgambo wa Palestina, huku wakiendelea kuchunguza na kukagua nyumba ya mshambuliaji mmoja wa kipalestina anayedaiwa kuwauwa waisraeli watatu wiki iliyopita.

Mapema hapo jana wanajeshi wa Israel waliwapiga risasi wanawake wawili. Jeshi la Israel limesema mmoja alimchoma kisu na kumjeruhi polisi mjini Hebron na mwengine hakuwa na silaha lakini alipuuza onyo lililotolewa na jeshi alipoagizwa kusimama alipokuwa anakaribia kituo cha ukaguzi cha Bethlehem.

Israel yashutumiwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wapalestina

Wapalestina wakiwa katika maandamano katika Ukingo wa Magharibi Picha: JAAFAR ASHTIYEH/AFP/Getty Images

Kawaida washambuliaji wa Palestina hufanya mashambulizi karibu na vituo vya ukaguzi lakini Wapalestina pamoja na makundi ya kutetea haki za binaadamu wanadai jeshi la Israel linatumia nguvu kupita kiasi na mara nyengine linawajeruhi na kuwauwa watu ambao hawana hatia.

Wajumbe wa kidiplomasia wa Umoja wa Ulaya kwa ajili ya Palestina wameishutumu Israel pia kutumia nguvu kupita kiasi kwa kumpiga risasi mwanamke ambaye hakuwa amejihami kwa silaha yoyote. Wameandika katika ukurasa wao wa Twitter kwamba tukio hilo ni lazima lichunguzwe na waliohusika kuwajibishwa.

soma zaidi: Israel yatikiswa na wimbi la mauaji

Huu ukiwa ni mgogoro wa hivi karibu unaofukuta wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Ramadhani ya mwaka huu imekwenda sambamba na siku tukufu kwa waumini wa Kiyahudi na Wakristo. Maandamano na vurugu wakati wa mwezi wa Ramadhani uliomuhimu kwa waumini wa Kiislamu mwaka uliopita ulisababisha mapigano ya siku 11 kati ya Isarel na wanamgambo wa Gaza.

Israel imeongeza shughuli zake za kijeshi katika ukingo wa Magharibi baada ya washambuliaji wa kipalestina kuwauwa waisraeli 14 katika mashambulizi manne ndani ya Israel katika wiki za hivi karibuni. Lakini wakati huo huo kumefanyika juhudi kadhaa kurejesha hali ya utulivu ikiwemo maelfu ya Wapalestina kutoka Gaza kufanya kazi ndani ya Israel.

Chanzo: ap/dpa