1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Jeshi la Israel laishambulia miji ya Rafah na Nuseirat

31 Mei 2024

Vikosi vya Israel leo vimeushambulia mji wa Rafah ulioko ukanda wa Gaza licha ya shutma kutoka jamii ya kimataifa kutokana na wasiwasi juu ya usalama wa raia.

Moshi unaofukuta baada ya mashambulizi ya anga ya Israel katika kambi ya wakimbizi ya Jabaliya, kaskazini mwa ukanda wa Gaza.
Moshi unaofukuta baada ya mashambulizi ya anga ya Israel katika kambi ya wakimbizi ya Jabaliya, kaskazini mwa ukanda wa Gaza. Picha: Abdul Rahman Salama/Xinhua/picture alliance

Vyanzo vya matibabu katika hospitali ya Deir al-Balah na katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat vimeeleza kuwa mashambulizi ya Israel yamesababisha vifo vya watu 11 usiku wa kuamkia leo.

Jeshi la Israel limesema askari wake wanaendelea na kile walichokiita "oparesheni maalum" katika mji wa Rafah na kwamba wamepata silaha ikiwemo mabomu yaliyofichwa ndani ya mahandaki katikati ya mji huo.

Jeshi hilo limeendelea kueleza kuwa mashambulizi yao ya anga yamewaua magaidi kadhaa waliokuwa karibu na eneo hilo, bila ya kufafanua zaidi.

Soma pia: Israel kuendeleza vita Gaza hadi mwishoni mwa mwaka 2024

Kuhusu oparesheni ya kijeshi inayoendelea mjini Rafah, msemaji wa serikali ya Israel David Mencer amesema, "Tayari tumewaangamiza karibu magaidi 300 mjini Rafah hadi sasa. Baadhi yao walikuwa wamejificha kwenye mahandaki, askari wetu walipigana nao kwa ujasiri tena chini ya hali ngumu mno. Tumepoteza pia baadhi ya askari wetu."

Hayo yanatokea baada ya shambulizi lililosababisha moto na kuua watu kadhaa katika kambi ya wakimbizi mwishoni mwa juma na kuzua wimbi jipya la shutma dhidi ya serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

Jeshi la Israel liliuvamia mji wa Rafah mapema mwezi Mei licha ya pingamizi ya jamii ya kimataifa kutokana na wasiwasi juu ya usalama wa raia waliotafuta hifadhi katika mji huo unaopakana na Misri.

Misri yakanusha kukubaliana na Israel kufungua kivuko cha Rafah

Malori ya misaada yameegesha kwenye kivuko cha mpaka wa Rafah yakisubiri kukaguliwa kabla ya kuingia ndani ya ukanda wa Gaza.Picha: REUTERS

Ama kwa upande mwengine, jeshi jilo limesema leo kuwa askari wake wamemaliza oparesheni zao mashariki mwa Jabaliya upande wa kaskazini mwa ukanda wa Gaza. Katika oparesheni hiyo, IDF imeweka wazi kuwa imeharibu kilomita 10 ya mahandaki na kiwanda kidogo cha kutengeneza silaha baada ya siku kadhaa za mapigano.

Katika oparesheni hiyo, askari wa Israel wameripoti kupata miili saba ya mateka.

Wakati hayo yanaripotiwa, Misri imekanusha kwamba imekubaliana na Israel kufungua kivuko muhimu cha mpaka wa Rafah.

Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Ukanda wa Gaza

02:51

This browser does not support the video element.

Ikinukuu chanzo kinachofahamu juu suala hilo kwa undani, shirika la habari la Misri la al-Qahera limeripoti leo kuwa "hakuna ukweli wowote” juu ya ripoti za baadhi ya vyombo vya habari kuhusu makubaliano kati ya Misri na Israel ya kufungua tena kivuko cha Rafah.

Soma pia:Baraza la usalama laitisha kikao cha dharura kujadili Rafah 

Chanzo hicho badala yake kimesisitiza kuwa, Misri inahimiza kuondoka kwa vikosi vya Israel katika kivuko hicho kama moja ya masharti ya kukifungua kivuko cha Rafah.

Mapema mwezi huu, Israel ilichukua udhibiti wa kivuko cha Rafah kinachopakana na Misri kwa upande wa Gaza, hatua ambayo ilikwamisha usafirishaji wa misaada muhimu ya kibinadamu kuingizwa ndani ya Gaza.

Tangu kufungwa kwa kivuko hicho, Misri imeshikilia msimamo wake kwamba kamwe haitoruhusu wala kuratibu kupitishwa kwa misaada kupitia mpaka huo hadi wanajeshi wa Israel watakapoondoka.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW