1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Israel lamuokoa mateka kusini mwa Gaza

27 Agosti 2024

Jeshi la Israel limemuokoa mtu mmoja aliyekuwa miongoni mwa watu wengi waliotekwa nyara katika shambulizi la Hamas la Oktoba 7.

Wanajeshi wa Israel wakiwa kusini mwa Ukanda wa Gaza
Wanajeshi wa Israel wakiwa kusini mwa Ukanda wa GazaPicha: Jack Guez/AFP

Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari amesema Jumanne kuwa Qaid Farhan Alkadi, mwenye umri wa miaka 52 ameokolewa katika handaki la chini ya ardhi wakati wa "oparesheni ngumu ya uokozi " kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Kulingana na Hagari, mateka huyo amepelekwa hospitali, ingawa hali yake ya kiafya ni nzuri.

Usalama wa mateka wanaoshikiliwa ni muhimu

Jeshi hilo limeandika kupitia jukwaa la mtandao la Telegram kuwa haliwezi kutoa taarifa zaidi kutokana na kuzingatia usalama wa mateka ambao bado wanashikiliwa, usalama wa vikosi vyake na usalama wa taifa.

Alkadi, anatoka jamii ya watu wachache ya Waarabu Wabedui wa Israel, na alikuwa akifanya kazi kama mlinzi katika kiwanda cha kupakia bidhaa huko Kibbutz Magen, mojawapo ya jamii za wakulima ambazo zilishambuliwa Oktoba 7.

Qaid Farhan Alkadi, mateka aliyekombolewa na vikosi vya IsraelPicha: The Hostages Families Forum/AP/picture alliance/dpa

Rais wa Israel, Isaac Herzog amesema kuokolewa mateka huyo ni wakati wa furaha kwa taifa la Israel na jamii ya Waisraeli kwa ujumla.

Wakati huo huo, Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kiutu, OCHA, Jens Laerke, amesema amri za mara kwa mara zinazotolewa na jeshi la Israel za kuwaondoa watu wengi Gaza, zinakwamisha shughuli za kutoa misaada, na hivyo kuwanyima Wapalestina haki yao ya kupata misaada na huduma za afya zinazohitajika sana.

Amri imetolewa kwa maeneo yanayowahifadhi watu 8,000

"Tangu Ijumaa, jeshi la Israel limetoa amri mpya mara tatu kuwataka Wapalestina kuondoka katika zaidi ya vitongoji 19 kaskazini mwa Gaza na Deir al Balah, huku zaidi ya watu 8,000 wasio na makaazi wakiishi kwenye maeneo hayo," alifafanua Laerke.

Msemaji huyo wa OCHA amesema hilo linafanya jumla ya idadi ya amri zilizotolewa za kuwaondoa watu wengi katika mwezi huu wa Agosti pekee kuwa 16.

Laerke amewaambia waandishi habari mjini Geneva kuwa wengi wa Wapalestina wanaolazimika kuondoka, tayari wanaishi kwenye maeneo ya watu walioyakimbia makaazi yao kutokana na mapigano.

Wapalestina wakiwa wanaelekea Bureij, GazaPicha: Hatem Moussa/AP Photo/picture alliance

Kulingana na OCHA, utoaji wa misaada kwenye eneo hilo ni mdogo kwa sababu za kiusalama na imekuwa vigumu eneo hilo kufikika.

Nalo Shirika la Afya Duniani, WHO limesema vituo vya afya vinapotelekezwa, uporaji mkubwa unatokea. Msemaji wa WHO, Dokta Margaret Harris amesisitiza kuwa vifaa vingi vya hospitali vinaibwa kila wakati, na mara nyingi hospitali zinaharibiwa kwa mashambulizi.

Soma zaidi: Mashambulizi ya Israel yauwa watu 18 Gaza

Huku hayo yakijiri, maafisa wa afya wa Palestina wamesema mashambulizi ya Israel yamewaua watu tisa katika maeneo ya Bureij na Maghazi, kambi mbili za kihistoria za wakimbizi kati ya nane huko Gaza, huku shambulizi jengine likiwaua watu watano huko Khan Younis, na shambulizi la tatu likiwauwa watu watatu huko Rafah.

 

(AFP, AP, DPA, Reuters)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW