1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMamlaka ya Palestina

Jeshi la Israel laonya kutumia 'nguvu zisizo mfano' Gaza

19 Septemba 2025

Jeshi la Israel limeonya kutumia nguvu zisizo mfano kwenye Jiji la Gaza, likirejelea wito wa kuwataka wakaazi kuhama, huku wakaazi nao wakijikuta hawana manusura popote walipo.

Gaza, Israel, Hamas
Wakaazi wa Jiji la Gaza wakijaribu kukimbia kunusuru maisha yao dhidi ya uvamizi wa jeshi la Israel siku ya Ijumaa (Septemba 19, 2025).Picha: Eyad Baba/AFP/Getty Images

Akiandika kupitia mtandao wa X, msemaji wa jeshi la Israel anayezungumza kwa Kiarabu, Avichay Adraee, alisema kwamba kiasi cha wakaazi 480,000 wa Jiji hilo tayari walikuwa wameshakimbia na kwamba jeshi sasa lingelitumia nguvu zisizo mfano dhidi ya wapiganaji wa Hamas na makundi mengine. 

Israel imekuwa ikilishambulia Jiji la Gaza  kwa mashambulizi ya anga na mizinga kwa dhamira ya kulitwaa kabila jiji hilo, ikiwa ni mwaka wa pili sasa tangu vita hivyo vilivyougeuza Ukanda wa Gaza kuwa magofu na wakaazi wake maiti, majeruhi ama wakiwa kwenye ukingo wa baa la njaa, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa unakisia kuwa Jiji la Gaza linakaliwa na watu milioni moja, na ikiwa kauli ya msemaji huyo wa jeshi la Israel ni ya kweli, hiyo inamaanisha kwa wastani nusu ya wakaazi hao hawapo tena.

'Hakuna palipo salama'

Hata hivyo, sehemu kubwa ya wakaazi wa Jiji hilo wanaripotiwa kukaidi amri ya kuhama iliyotolewa na Israel, wakihoji kuwa hapana mahala palipo salama ndani ya Ukanda mzima wa Gaza.

Wakaazi wa Jiji la Gaza wakijaribu kukimbia kunusuru maisha yao dhidi ya uvamizi wa jeshi la Israel siku ya Ijumaa (Septemba 19, 2025).Picha: Mahmoud Issa/REUTERS

"Hatupajui pa kwenda. Wanatuambia twende kusini, Muwasi. Sina hema, sina pesa ya kukodi gari. Hakuna mmiliki wa gari aliyekubali kunichukuwa. Sasa mtu kama miye aende wapi na sina pesa, wala hema wala gharama za usafiri? Mtu hata watoto wake wanamshinda kuwalisha kwenye hali hii." Alisema Zuheir Daban, mmoja wa Wapalestina hao.

Kwa wengine, kama Sanaa Sobh, mwanamke mtu mzima na mgonjwa wa saratani, alijaribu kuondoka lakini bado analalamikia madhila na mateso anayokumbana nayo.

"Ni maisha ya motoni, lakini kwa nini yote haya? Tumewafanya nini hadi watufanye hivi? Tunafukuzwa, twende wapi? Kosa letu nini? Watoto wetu wamewakosea nini? Mimi nauguwa saratani. Kosa langu ni lipi hadi niteswe hivi? Je, hili si jambo la fedheha kwao?" Alisema mwanamke huyo.

Marekani yaunga mkono uvamizi wa Gaza

Vifaru vya Israel vikiingia kwenye Jiji la Gaza siku ya Ijumaa (Septemba 19,2025).Picha: Ammar Awad/REUTERS

Uvamizi huo wa jeshi la Israel dhidi ya Jiji la Gaza unaoungwa mkono na Marekani unafanyika wakati jopo la uchunguzi la Umoja wa Mataifa likiituhumu Israel kwa kufanya mauaji ya kimbari kwenye Ukanda wa Gaza, na kuwanyooshea kidole cha lawama moja kwa moja Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na maafisa wengine wa ngazi za juu kwa kuchochea uhalifu huo.

Israel imekataa matokeo ya uchunguzi huo na kuyaita upotoshaji na uongo.

Siku ya Alkhamis (Septemba 18), Marekani kwa mara nyengine tena ilipiga kura ya veto  kuzuwia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokuwa liagize usitishaji wa mapigano, ikiendeleza utamaduni wake wa kila siku kuilinda Israel dhidi ya shinikizo la kimataifa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW