Jeshi la Israel lasema miili iliyorejeshwa sio ya mateka
1 Novemba 2025
Jeshi la Israel limesema leo kwamba miili mitatu iliyopokelewa jana kutoka Gaza kupitia shirika la Msalaba Mwekundu sio ya mateka waliokuwa wakishikiliwa eneo la Palestina.
Jeshi hilo limelieleza shirika la habari la AFP kwamba uchunguzi wa kitaalamu umegundua kuwa miili hiyo haikuwa ya mateka 11 waliofariki ambao bado wanatakiwa kukabidhiwa kwa Israel, chini ya makubaliano ya kusitisha vita yaliyosimamiwa na Marekani.
Kati ya miili 17 ambayo tayari imerejeshwa tangu kuanza utekelezaji wa makubaliano, 15 kati yake ni raia wa Israel, raia mmoja ni wa Thailand na mwingine ni wa Nepal.
Israel inaishutumu Hamas kwa kukiuka makubaliano hayo na kutorejesha miili ya mateka haraka, lakini kundi hilo linadai kwamba linahitaji muda kuitafuta miili iliyokwama chini ya vifusi.