1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yatoa agizo kwa wakaazi wa Baalbek, Lebanon kuhama

Hawa Bihoga
3 Novemba 2024

Jeshi la Israeli, IDF, limewataka wakaazi wa mkoa wa Baalbek, mashariki mwa Lebanon, kuondoka, likijiandaa kwa mashambulizi dhidi ya maeneo ya Hezbollah huko Baalbek na Douris.

Lebanon | Wanajeshi wa Israel wakiwa katika uwanja wa vita
Wanajeshi wa Israel wakiwa katika uwanja wa vita LebanonPicha: Ilia Yefimovich/dpa/picture alliance

Hii ni baada ya ving'ora kuanza kulia kwenye mpaka wa Israeli kutokana na kurushwa kwa roketi kutoka Lebanon. 

IDF inaendeleza mashambulizi makhsusi kusini mwa Lebanon ili kuwaangamiza wapiganaji wa Hezbollah na imedai kuzuwia makombora kadhaa yaliofyatuliwa nchini Israel, huku mengine yakianguka katika maeneo ya wazi.

Mashambulizi ya karibuni ya roketi kutoka Lebanon yalisababisha vifo saba katika eneo la Metula nchini Israel.

IDF imedai pia kugundua idadi kubwa ya silaha kusini mwa Lebanon na kukabiliana na kile ilichokiita magaidi. Tangu Septemba 23, mzozo huo umesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,900 nchini Lebanon na vifo vya wanajeshi 38 wa Israeli. 

Soma pia:Khamenei aapa kuishambulia tena Israel, Marekani yaonya

Mzozo uliongezeka baada ya Hezbollah kuanza kurusha makombora mnamo Oktoba 8 katika hatua ya kuiunga mkono Hamas, kufuatia shambulio lake dhidi ya Israeli Oktoba 7 2023, ambalo lilisababisha vifo vya watu 1,206 nchini Israeli.

Majibu ya kijeshi ya Israeli katika Ukanda wa Gaza yamesababisha vifo vya Wapalestina 43,341, wengi wao wakiwa raia.