Israel yazuia msafara wa meli ya misaada kuelekea Gaza
2 Oktoba 2025
Msafara huo, ujulikanao kama Global Sumud Flotilla (GSF), ulikuwa na takriban meli 45 zilizobeba wanasiasa na wanaharakati, na uliondoka Uhispania mwezi uliopita kwa lengo la kuvunja mzingiro wa kijeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza - eneo ambalo Umoja wa Mataifa umetahadharisha kwamba linakabiliwa na njaa kali.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imethibitisha kuwa meli kadhaa za GSF zimezuiwa na abiria wake kuhamishwa hadi bandari ya Israel.
Kwa upande wake, GSF imeeleza kuwa hatua ya kuzuiwa kwao ni kinyume cha sheria za kimataifa, na wala sio kitendo cha kujilinda kama inavyodai Israel, bali ni "kitendo cha kukata tamaa kwa dhahiri."
Kupitia mitandao ya kijamii, msafara huo umeandika: "Hali hii inaonyesha wazi jinsi gani Israel inavyokwenda mbali kuhakikisha Gaza inaendelea kuwa na njaa na kutengwa."
Kundi la Hamas ambalo shambulio lake la Oktoba 7, 2023 dhidi ya Israel lilichochea vita vya Gaza, limelaani hatua ya kuzuiwa kwa msafara huo katika maji ya kimataifa, na kuitaja hatua hiyo kama "uhalifu wa uharamia na ugaidi wa majini."