1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Kiafrika laanza kuchukua nafasi ya Wafaransa Mali

24 Januari 2013

Wanajeshi wa Kiafrika wanasonga mbele kuelekea katikati ya Mali huku kukiwa na taarifa za jeshi la Mali kufanya mauaji ya makusudi na uvunjaji wa haki za binaadamu dhidi watu wa jamii za Kiarabu na Kituareg.

Mwanajeshi wa Mali
Mwanajeshi wa MaliPicha: Reuters

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius, kikosi cha mwanzo cha wanajeshi wa Afrika "tayari kimeanza kuelekea miji ya kati".

Fabius amesema kwamba ametiwa moyo sana na ukweli kwamba kikosi hicho kimesonga mbele kwa haraka zaidi kuliko ilivyokuwa imetarajiwa, licha ya kwamba mafanikio hayo ya haraka yanaweza kusababisha ugumu mwengine, ukiwemo wa vifaa na fedha.

Afisa mmoja kutoka wizara ya ulinzi ya Mali amethibitisha kuwasili kwa wanajeshi 160 wa Burkina Faso kwenye mji wa Markala, ulio umbali wa kilomita 270 kaskazini mwa mji mkuu, Bamako, na wenye daraja muhimu la Mto Niger.

Kwa mujibu wa afisa huyo, tayari wanajeshi hao wamechukua nafasi ya jeshi la Ufaransa na sasa wanaelekea miji ya Niono na Diabaly iliyoko kaskazini kabisa mwa Mali.

Kikosi cha wanajeshi 1,000 kutoka mataifa ya Afrika ya Magharibi na Chad kinadhamiria kuchukuwa nafasi ya wanajeshi wa Ufaransa wanaoongoza sasa operesheni dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu.

Umoja wa Mataifa uliidhinisha kupelekwa kwa wanajeshi 3,300 chini ya usimamizi wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika ya Magharibi, ECOWAS, lakini kuhusika kwa Chad, ambayo imeahidi kutuma wanajeshi 2,000, kunamaanisha kikosi hicho kinaweza kuwa kikubwa zaidi.

Yayi akutana na Merkel

Hapo jana, Rais Thomas Boni Yayi wa Benin, ambaye ndiye pia mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika na ambaye nchi yake pia imepeleka wanajeshi nchini Mali, alikuwa na mazungumzo na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani mjini Berlin, juu ya suala hilo.

Rais Thomas Bonuses Yayi wa Benin.Picha: K.Sia/AFP/Getty Images

"Kansela Merkel ameahidi Ujerumani itaongeza ushiriki wake kutoka ulivyo sasa na pia ameahidi ushiriki wa Ujerumani kwenye mkutano wa wafadhili juu ya Mali mwishoni mwa mwezi wa Januari." Alisema Rais Boni Yayi baada ya mkutano huo.

Kansela Merkel, kwa upande wake, amesema Ujerumani inatekeleza jukumu lake kwa Mali kama ilivyoahidi.

"Ujerumani inashughulika na usafirishaji wa wanajeshi, lakini pia kwenye suala la vifaa na mafunzo kwa wanajeshi wa Mali. Na kwa upande wake Rais Boni Yayi ameweka bayana kwamba atafanya kila awezalo kuhakikisha kuwa tatizo hili linatatuliwa haraka iwezakanavyo. Na tumekubaliana kuchukua hatua hizo haraka sana."

Wanajeshi wa Mali wafanya mauaji ya makusudi

Wakati hayo yakiripotiwa, kuna taarifa za jeshi la Mali kufanya mauaji ya makusudi na uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu dhidi ya watu wenye asili ya Kiarabu na Kituareg kwenye maeneo yanayokimbiwa na wapiganaji wa Kiislamu.

Wanajeshi wa Nigeria nchini Mali.Picha: AP

Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binaadamu limesema katika mji wa kati wa Sevare, watu 11 waliuawa kwenye kambi moja ya kijeshi karibu na kituo cha mabasi na hospitalini. Taarifa za uhakika zinasema kiasi cha watu 20 wameuliwa kwenye eneo hilo hilo na miili yao kutupwa visimani au kuharibiwa kabisa.

Visa kama hivyo vimeripotiwa pia kwenye miji ya Noino na Siribala. Shirika hilo limetaka uchunguzi huru ufanyike juu ya visa hivyo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman