Jeshi la Kongo laanzisha 'awamu ya mwisho' ya kuwang'oa M23
1 Novemba 2013Mkaazi mmoja wa mji wa Jomba ulio mpakani mwa Kongo na Uganda, ameliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu kwamba sasa "wanajeshi wa Kongo wanaendesha operesheni zao dhidi ya waasi"kwenye eneo hilo.
Mkaazi huyo aliyekataa kutaja jina lake amesema amemuona msichana mmoja akiwa amejeruhiwa kwa risasi katika mapigano ya hivi karibuni kabisa, ingawa hakufafanua zaidi. "Wanajeshi wa serikali walitumia usiku wao (wa kuamkia Ijumaa ya tarehe 1 Novemba) hapa na sasa wamekwenda mstari wa mbele wa mapigano," amesema mtu huyo.
Shirika la habari la AFP limeripoti kwamba hata wakati wa mazungumzo hayo ya simu, milio ya risasi ilikuwa inasikikana waziwazi, ambapo chanzo hicho cha habari kilisema kwamba pande zote mbili za mapigano zilikuwa zikitumia silaha nzito. Mwandishi wa AFP aliyeko upande wa Uganda aliweza pia kusikia milio hiyo ya risasi.
MONUSCO yasaidia
Chanzo kimoja kutoka Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo (MONUSCO), ambacho kinalisaidia jeshi, amesema mashambulizi hayo dhidi ya M23 ni "awamu ya mwisho," baada ya jeshi hilo kukichukua kituo kikuu cha waasi cha Bunagana hapo Jumatano.
Lakini wapiganaji wenye msimamo mkali wa M23, wanaokisiwa kufikia 100, wanasemekana kujificha kwenye eneo hilo lenye milima mitatu umbali wa kiasi cha kilomita 80 kaskazini mwa mji wa Goma, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kivu ya Kaskazini.
"Jeshi la Kongo limewazunguka wapiganaji hawa wachache wa M23 ili kuwamaliza. Operesheni inaendelea," kilisema chanzo hicho.
Tangu mapigano kuanza tena mnamo tarehe 25 Oktoba, baada ya mazungumzo ya amani kuvunjika nchini Uganda, hakuna wanajeshi wa Umoja wa Mataifa waliojihusisha moja kwa moja kwenye mashambulizi, lakini MONUSCO imekuwa ikiwasaidia wanajeshi wa serikali kwa taarifa za kiintelijensia na vifaa.
Kabila awataka M23 wajisalimishe
Baada ya waasi kupoteza makao yao makuu ya Bunagana, siku ya Jumatano Rais Joseph Kabila aliwasihi tena wapiganaji hao wa M23 kusalimu amri kwa hiyari, akiwaonya kwamba wakishindwa kufanya hivyo, basi wanajeshi wake wangeliwalazimisha.
Maelfu ya watu wamekimbia mapigano kati ya wanajeshi wa serikali na wapiganaji wa kundi la M23, ambalo limeundwa na waasi wa zamani wa Kitutsi waliokuwa wameingizwa kwenye jeshi la Kongo chini ya makubaliano ya amani ya mwaka 2009, lakini kisha wakaasi mwezi Aprili 2012, wakidai kwamba makubaliano hayo hayakuwa yametekelezwa kikamilifu.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf