Jeshi la Kongo latangaza kuuchukuwa tena mji wa Masisi
9 Januari 2025Wakiungwa mkono na wapiganaji vijana Wazalendo, wanajeshi tiifu kwa serikali ya Kongo walisonga mbele kwa kuzishambulia ngome za M23, siku nzima ya Jumatano katika mji mkuu wa Masisi ambako wameweka kambi hadi leo Alhamisi. Kulingana na vyanzo kadhaa, Jeshi la Kongo FARDC, lilifanikiwa kuuteka mji huo baada ya waasi wa M23 kukimbia wakielekea kwenye mlima wa Kahongole ulioko kwenye mji huo wa kimkakati, na ambako FARDC ilikuwa ikirushia mizinga kwa kuwasambaratisha waasi hao hadi jana jioni. Raia mmoja aliyeshuhudia tukio hilo, na ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa sababu za kiusalama, anaelezea zaidi.
"Baada ya mapigano hayo yaliyowafanya kuuchukua mji wa Masisi, waliendelea hadi mji mdogo wa Lushebere, lakini walikutana na kizuizi Katale ambako walilazimika kutumia mashambulizi ya ndege. Nathibitisha kwamba FARDC wameukamata mji wa Masisi."
Wapiganaji Wazalendo wanaoliunga mkono jeshi la Kongo, walizidisha mashambulizi yao pia kwenye kijiji cha Mashaki uliko takribani kilomita tano, kutoka mji wa Katale unaokaliwa na M23 wiki moja sasa.
"Tunaona Wazalendo wamewasili hapa"
Hali ilikuwa ya wasiwasi kwa wakaazi waliokwama kwenye mji huo baada ya jeshi la Kongo na washirika wake kuvurumisha mizinga kwenye ngome za waasi hao wanaosaidiwa na jeshi la Rwanda.
Video inayozunguka kwenye mitandao ya kijamii, inaonesha idadi ndogo ya wakazi wa mji wa Ngungu wilayani Masisi, wakishangilia ujio wa jeshi la Kongo baada ya M23 kukimbia.
"Tunamshukuru Raisi wetu Felix Tshisekedi, tunaona Wazalendo wamewasili hapa Ngungu, tumefurahi sana kuona jinsi serikali ilivyochukuwa udhibiti wa mji wa Ngungu."
Jeshi laapa kuyakomboa maeneo yote ya Kivu
Hata hivyo, katika mkutano wao jana Jumatano huko jijini Kinshasa, maafisa wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, waliapa kuyakomboa maeneo yote yanayokaliwa na waasi ambao hadi sasa wamechukua maeneo makubwa yenye utajiri wa maliasili katika jimbo la Kivu Kaskazini. SUKISA NDAYAMBAJE ni naibu kiongozi wa mpango wa upokonyaji silaha mashariki mwa Kongo.
"Iwapo tunahitaji amani ni lazima tuungane mkono ili tumuonyeshe Raisi Paul Kagame kwamba Kongo ni yetu na kuweka wazi utofauti kati ya Mhutu wa DRC na wa Rwanda. Kwa wale Wahutu wa Rwanda watapita kwenye mchakato wa makubaliano ya Luanda na hao Wahutu wa Kongo wataendelea na shughuli zao kama kawaida. Ni vyema kuweka wazi tofauti kati ya makabila hayo mawili."
Katika tangazo lao hiyo jana, waasi wa M23 wameituhumu serikali ya Kongo kwa kile walichokitaja kama ukiukwaji wa mikataba ya usitishwaji mapigano, saa chache tu baada ya jeshi la Kongo lilipochukua udhibiti wa miji ya Masisi na Ngungu.