Jeshi la Lebanon laanza kupeleka askari kusini mwa nchi hiyo
27 Novemba 2024Ni baada ya Waziri Mkuu Najib Mikati kutangaza uamuzi wa baraza la mawaziri wa kuimarisha uwepo wake katika eneo hilo kufuatia makubaliano ya kusitishwa mapigano kati ya Hezbollah na Israel. Mpango huo wa usitishaji mapigano uliosimamiwa na Marekani na Ufaransa, ulianza kutekelezwa leo na mpaka sasa unaonekana kuheshimiwa. Wakaazi wameonekana wakisafiri kwenye magari yaliyojaa mali zao kurudi kusini mwa Lebanon. Kama utaheshimiwa kikamilifu, utafikisha mwisho karibu miezi 14 ya mapigano kati ya Israel na Hezbollah. Msemaji wa jeshi la Israel amethibitisha mpango wa askari wao kuanza kuondoka Lebanon katika siku 60 kama sehemu ya makubaliano hayo. Amewaambia waandishi kuwa ni mchakato utakaofanyika kwa hatua. Hata hivyo, amesema hiyo itategemea tu na kama wanamgambo wa Hezbollah, wanaoungwa mkono na Iran watayaheshimu makubaliano yaliyofikiwa.