Jeshi la Mali laukamata mji wa Konna
18 Januari 2013Baada ya mapigano makali kati ya wanajeshi wa serikali na waasi, hatimaye vyanzo vya kijeshi na usalama vinathibitisha kuanguka kwa mji wa Konna kutoka mikononi mwa kundi la Ansar Dine hivi leo.
Hapo awali, jeshi la Mali ilikuwa imeripoti kwamba lilshaudhbiti mji huo, lakini taarifa hizo zikakanushwa na Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian, ambaye alisema kwamba bado eneo hilo lilikuwa mikononi mwa waasi wa Kiislamu.
Tangu mwezi Aprili mwaka jana, makundi ya waasi yamekuwa yakilidhibiti eneo zima la kaskazini mwa Mali na pia kuuchukua mji huo wa Konna ulio umbali wa kilomita 700 kutoka mji mkuu, Bamako, hatua ambayo inasemekana kuilazimisha Ufaransa kuingilia kati kijeshi mapema mwezi huu.
Wanajeshi wa ECOWAS wawasili
Kuchukuliwa kwa mji wa Konna kutoka mikononi mwa waasi, kumesadifiana na kuwasili kwa maelfu ya wanajeshi wa Afrika ya Magharibi nchini Mali, kusaidiana na vikosi vya Mali na Ufaransa kukabiliana na waasi katika maeneo ya jangwa kaskazini mwa nchi hiyo. Tayari Ufaransa imeongeza wanajeshi wake kufikia 1,400 na pia kutuma helikopta za kijeshi kukisaidia kikosi chake maalum huko.
Kwa upande mwengine, hapo jana Umoja wa Ulaya ulikubali kuanzisha kikosi cha mafunzo kufikia mwezi Februari kwa ajili ya Mali. Tayari Ujerumani ilishapeleka ndege mbili za kijeshi kwa ajili ya kusaidia kuwasafirisha wanajeshi wa ECOWAS, ingawa Waziri wa Mambo ya Nje, Guido Westerwelle, amesisitiza kwamba mataifa ya Afrika yanapaswa kuachiwa fursa ya kutatuta mizozo yake yenyewe.
"Jambo la muhimu zaidi tunalopaswa kulifanikisha, ni kwa mataifa ya Kiafrika kuwa na dhamana na uwezo wa kushughulikia matatizo yake." Alisema Westerwelle akiwa mjini Brussels, Ubelgiji, baada ya mkutano wa Umoja wa Ulaya juu ya Mali.
Ufaransa inakabiliwa na vita vya muda mrefu?
Hata hivyo huku hayo yakiarifiwa vikosi jeshi la Ufaransa vilivyoko nchini Mali vitatoa changamoto kwa bajeti ya Ufaransa ambayo ilikuwa inatarajiwa kupumua kidogo kutokana na kuondoka kwa vikosi vyake nchini Afghanistan.
Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian, alipoulizwa ni kwa muda gani vikosi vya Ufaransa vitabakia nchini Mali kupambana na waasi, alisema kuwa hana jibu kamili la swali hilo lakini akakiri kwamba itachukua muda mrefu kuwaondoa waasi katika eneo la kaskazini kwa sababu waasi hao wamejikita katika eneo la kaskazini.
Bajeti ya wizara ya ulinzi kwa maswala ya nje kwa mwaka wa 2013 ni euro milioni 630 hii ikiwa imepungua kwa milioni 90 ikilinganishwa na mwaka uliopita, wakitarajia wataweka akiba kutokana na kuondolewa kwa majeshi hayo nchini Afghanistan.
Kwa sasa Mali inapokea msaada wa ndege za kubeba majeshi kutoka Ubelgiji, Uingereza, Canada, Denmark, Ujerumani na Marekani. Ufaransa na mataifa mengine ya Afrika yanachangia pia vikosi vya wanajeshi.
Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo