Jeshi la Myanmar ladai kwamba halikuipindua serikali
16 Februari 2021Jeshi la Myanmar limeitaja hatua yake ya kuchukua kwa nguvu madaraka kwamba ni halali na haiwezi kuitwa mapinduzi kwasababu suala la wizi wa kura katika uchaguzi wa Novemba halikushughulikiwa na hivyo hatua hiyo ilistahiki. Lakini jeshi hilo pia limesema litayarudisha madaraka kwa chama kitakachopata ushindi baada ya kufanyika uchaguzi mpya.
Brigedia jenerali Zaw Min Tun ambaye ni msemaji wa serikali hiyo ya kijeshi akizungumza katika mkutano wa kwanza na waandishi habari tangu jeshi litwae madaraka amesema lengo lao ni kuandaa uchaguzi na kuyakabidhi madaraka kwa yoyote atakayeshinda ingawa jeshi hilo halikutangaza tarehe ya uchaguzi huo mpya lakini imetangaza hali ya dharura kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Kwa upande mwingine maandamano ya amani ya wamyanmar wanaoipinga hatua ya jeshi ya mapinduzi yamerudi tena mitaani hii leo baada ya kushuhudiwa vurugu kubwa dhidi ya waandamanaji hao hapa jana Jumatatu. Vurugu hizo zilifanywa na vikosi vya usalama huku pia huduma za Internet zikiwa zimefungwa kwa siku ya pili mfululizo.
Maandamano hayo yameanza kushuhudiwa mapema kabisa katika mji wa kibiashara wa Yangon na miji mingine ya nchi hiyo ambapo waandamanaji wanadai kiongozi aliyechaguliwa na wananchi Aung San Suu Kyi na maafisa wa serikali yake waliokamatwa waachiwe huru. Watawa wakibudha nao wameandamana nje ya ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini humo huku waandamanaji wengine wakiilenga benki kuu ambako polisi wameifunga barabara iliyoko kwenye eneo hilo la benki kuu.Suu Kyi kuendelea kuzuiliwa wakati maandamano yakiendelea
Ikumbukwe kwamba jeshi la Myanmar limezuia mikusanyikao ya watu zaidi ya watano na waandamanaji wanaonesha kuikaidi amri hiyo. Takriban waandamanaji 3000 wengi wao wakiwa wanafunzi wamejitokeza pia katika mitaa ya mji wa Mandalay mji wa pili kwa ukubwa nchini humo,wakiwa wamebeba mabango yenye sura ya Suu Kyi ,wakisikika wakidai Demokrasia irudishwe nchini Myanmar.
Hata hivyo kuna polisi wachache walioonekana wakiyazunguka maandamano hayo huku wengi wa askari wakiripotiwa kuonekana kuyalinda hasa majengo muhimu katika mji huo kama vile matawi ya mabenki ya serikali. Katika mji huo wa Mandalay jana Jumatatu polisi waliyavunja maandamano ya watu 1000 kwa kutumia nguvu na kuwashambulia waandamanaji kwa fimbo na kwa kutumia manati.
Vyombo vya habari vya Myanmar pia viliripoti kwamba risasi za mpira zilifyetuliwa na watu wachache walijeruhiwa kwenye vurugu hizo. Kadhalika gazeti moja nchini humo limeripoti kwamba baraza la kijeshi limejadili juu ya kuchukua hatua ya kuzima kile kinachoitwa serikali nyingine ya pembeni iliyoanzishwa na wabunge kadhaa wa chama cha San Suu Kyi, National League for democrasy waliozuiwa kuingia bungeni baada ya jeshi kulizuia bunge kufungua vikao vyake mnamo Februari mosi.